Bunge la Katiba Litaendelea Hata Bila Ukawa – Samuel Sitta

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Na Winner Abraham na Rose Masaka – MAELEZO, Dar es salaam

MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma. Alisema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.

Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.

“Kamati hiyo, imeamua kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalum la Katiba liendelee kwa sababu yapo masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Mambo mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano, haki za wakulima, wafugaji, wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,” alisema Sitta katika taarifa hiyo.

Aidha aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.

Alisema hatua ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.

Aliongeza kwamba Kamati hiyo, inaona kwamba kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.

Alisema Kamati hiyo inarejea kwamba wajumbe hao 629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.

“Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.

Mwenyekiti huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo,  uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu  zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.

Alisema Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi, walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.

“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti hadi asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema Sitta katika taarifa yake. 

Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye kuipigia kura Katiba mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.