Na Joachim Mushi
BUNGE Maalumu la Kujadili rasimu ya Katiba Mpya limepitisha kanuni zitakazotumika kuwaongoza wabunge hao katika kutekeleza kazi zao. Rasimu hiyo ya kanuni imepitishwa leo asubuhi mjini Dodoma kwa asilimia kubwa ya wajumbe wa bunge maalumu la katiba baada ya kuhojiwa na mwenyekiti wa muda wa bunge hilo, Bw. Pandu Amir Kificho.
Rasimu ya kanuni iliyopitishwa leo inatarajiwa kutumika kumuongoza Mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo atakayechaguliwa kesho na wajumbe wa bunge hilo. Hata hivyo vifungu vyote vya rasimu vimepitishwa isipokuwa kile cha upigaji wa kura kupitisha hoja na maamuzi mbalimbali ndani ya bunge hilo.
Awali akiwasilisha hoja ya kupitisha kanuni hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa muda wa Bunge juu ya undwaji wa rasimu ya kanuni, Profesa Costaric Mahalu alisema kamati yake imejitahidi kufanya kazi ya kupitia rasimu hizo na kuziweka kama ilivyokubaliwa na maelekezo ya wajumbe wa kamati na wajumbe wa bunge la katiba hivyo ziko tayari kufanya kazi iliyotarajiwa.
Aliwataka wabunge wote kukubaliana na kuziunga mkono ili bunge hilo maalumu sasa liendelee na kazi yake. Akizungumzia kipengele cha upigaji kura kwa wajumbe hao kilicho, Prof. Mahalu alisema kipengele hicho kitapitishwa baadaye baada ya wajumbe wote kukubaliana.
Akitoa ufafanuzi juu ya Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo, Bw. Kificho alisema uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika kesho saa kumi jioni ndani ya Bunge hilo hivyo kuwataka wanaotaka kugombea nafasi hilo wafike katika ofisi za bunge mjini Dodoma leo na kuchukua fomu zao ambazo watazirejesha kesho saa nne asubuhi katika ofisi hizo hizo.
Hata hivyo muda mfupi kabla ya kupitishwa kwa rasimu ya kanuni za bunge hilo, hali ya hewa ya ukumbu wa bunge ulichafuka ghafla baada ya mjumbe mmoja wa bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila kunyanyuka na kuanza kumtuhumu Kificho anapendelea baadhi ya wajumbe kwa kuwapa nafasi ya kuzungumza katika bunge hilo na kuwaacha wengine.
“…Hivi ni kwanini wewe mwenyekiti hutaki mimi nizungumze katika bunge hili, mungu amenipa uwezo na nafasi ya kuzungumza na kanuni zinaruhusi hivyo, naomba niambie kwanini hutaki kunipa nafasi mimi nizungumze…sema ili wote wasikie…,” alisema Mtikila baada ya kunyanyuka bila idhini ya mwenyekiti wa bunge wa muda.
Wabunge walishikwa na mshangao na wengine kuanza kupiga kelele huku wengine wakisikika wakimtuhumu mchungaji mtikila amekosa nidhamu kwa kiteto hicho. Mtikila aliendelea kuhoji hivyo hadi pale alipozimiwa kipaza sauti chake baada ya kukiuka utaratibu.
Kwa upande wake, Kificho alijitetea kuwa orodha ya watu walioomba kuzungumza kabla ya kupitisha rasimu ya kanuni ilikuwa ni ndefu hivyo hakukuwa na muda wa kila mmoja kupata nafasi ya kuzungumza. “…Naomba radhi kwa wale waliokosa nafasi ya kuchangia maana walioomba kuzungumza ni wengi sana hivyo si rahisi kila mmoja kupata nafasi,” alisema Kificho.