Bunduki haiwezi kumaliza matatizo yetu – JK

Malabo, Equatorial Guinea

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameziambia Sudan na Sudan Kusini kuwa bunduki haiwezi kutoa majawabu ya mvutano kati ya pande hizo ambazo zitatengana na kuwa nchi mbili tofauti Julai 9, mwaka huu, 2011, wakati Sudan Kusini itakapokuwa Taifa Huru.

Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa njia pekee ya kupata majawabu sahihi ya mvutano kati ya pande hizo ni kwao kuendelea kuzungumza na kutafuta suluhisho la amani la matatizo yao kwa njia ya majadiliano.

Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Juni 30, 2011, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan, Mheshimiwa Ali Osman Mohammed Taha wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika katika Kijiji cha kisasa kabisa cha AU cha Sipopo nje ya mji wa Malabo katika Kisiwa cha Bioko, Equatorial Guinea.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amewaambia kiongozi huyo wa Sudan: “bunduki haiwezi kuwa jibu kwa sababu hata mkipigana hatimaye mtalazimika kuzungumza. Hivyo, kama mnaweza kuzungumza na kukubaliana bila kupigana basi hilo ni bora sana.”

Kwenye mazungumzo hayo, kiongozi huyo wa Sudan amemwambia Rais Kikwete juu ya hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa kumaliza mzozo wa kisiasa na kiusalama ambao ulizuka kufuatia tukio la karibuni katika Jimbo la mpakani la Abyei ambalo mpaka sasa halitakuwa sehemu ya eneo la Sudan ama Sudan Kusini ifikapo Julai 9 na litabakia eneo linalojitegemea.

Katika mzozo huo, majeshi ya pande zote mbili yalipigana yakasababisha upotevu wa maisha na mali na kulazimisha mamia ya watu kukimbia eneo la mapigano, hatua ambayo ilizusha wasiwasi kuwa hali hiyo ingeweza kusababisha kuvunjika kwa Makubaliano ya Kuleta Amani katika Sudan ya Comprehensive Peace Agreement (CPA).

Katika mazungumzo ya leo, Makamu huyo wa Rais wa Sudan amemhakikishia Rais Kikwete kuwa Sudan itaheshimu makubaliano ya CPA ya kuiwezesha Sudan Kusini kuwa Taifa Huru ifikapo Julai 9, mwaka huu, 2011.

Kiongozi huyo wa Sudan amesema kuwa matatizo mengi ya mvutano kati ya pande hizo mbili yamepatiwa majawabu isipokuwa suala la mgawanyo wa mapato ya mafuta kati ya pande hizo mbili ambako pande hizo hazijafikia mwafaka.

Katika Sudan, mafuta huchimbwa katika eneo la Kusini mwa Sudan lakini husafirishwa kwa mabomba yanayopitia Sudan kwenda kwenye Bandari ya Port Said iliyoko eneo litakalobakia Sudan baada ya Julai 9.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini,

Malabo, Equatorial Guinea.

01 Julai, 2011