Bunda
HALMASHAURI ya Wilaya ya Bunda, inatarajia kufanya mazungumzo na uongozi wa wilaya hiyo, ili iruhusiwe kukusanya ushuru kwenye magari yanayofika katika kituo
cha Bunda, kwa ajili ya kupeleka watu kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila, Loliondo Arusha, kupata tiba ya mchungaji huyo.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na madiwani wa halmashauri hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti, Joseph Malimbe, kwenye kikao cha bajeti kilichofanyika, katika
Ukumbi wa Halmashuri mjini Bunda.
Madiwani hao wamepanga kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Isaac ili
wafanye mazungumzo na halmashauri kuruhusiwa kukusanya ushuru huo wa magari na fedha zitumike kuboresha masuala ya usafi, pamoja na kuweka miundombinu mizuri katika kituo hicho.
“Tutazungumza na Mkuu wa Wilaya yetu, maana wote ni Serikali tuzungumze namna ya
kuweza kukusanya ushuru kwenye kituo hicho…na ushuru huu utasaidia kuboresha
suala la usafi katika kituo hicho na pia suala zima la kuboresha miundombinu,”
alisema Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Joseph Malimbe.
Kwa sasa utaratibu uliopo ni kila gari inayopita katika kituo hicho inatozwa kiasi cha sh. 1,000 kwa ajili ya kupewa kibali cha kuruhusiwa kwenda Loliondo, mkoani Arusha, kwa Mchungaji mstaafu Mwasapila.
Wakati huo huo, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, limepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2011/12, kwa kukadiria kukusanya zaidi ya sh. bilioni 1.1 kutoka kwenye vyanzo vyake, pamoja na fidia ya vyanzo vilivyofutwa na Serikali Kuu.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Cyprian Oyier, Mweka
Hazina wa halmashauri hiyo, Peter Makuru alisema makisio ya bajeti mwaka 2011/12, yameandaliwa kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa kitaifa.
Makuru alisema halmashauri hiyo inakadiria kukusanya kiasi cha sh.
18,958,634,237, ikiwa ni ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara,
Na kiasi cha sh. 2,721,261,546 kama matumizi mengine huku sh. 6,523,535,378 zikitumika kwa miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo imepitishwa wakati tayari shirikisho la vyama vya wafanyakazi
vinavyofanya kazi na halmashauri hiyo, vimekwishatangaza kufanya maandamano
makubwa ya kuipinga kwa madai haikupitia kwenye Baraza la Wafanyakazi kama sheria inavyotamka.