BRN Yatekeleza Mengi Ndani ya Mwaka

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein naye amehudhuria semina hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein naye amehudhuria semina hiyo.


 
Na Mwandishi Wetu
 
MPANGO wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao Serikali ya Tanzania imeanza kuutekeleza tangu Julai, 2013 umeleta matokeo makubwa yatakayosaidia kukuza uchumi wa nchi na huduma kwa wananchi.
 
Hayo yalisemwa juzi visiwani Zanzibar na Mtendaji Mkuu kutoka Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekeleaji wa Miradi (PDB) inayosimamia utelezaji wa BRN kwa Tanzania Bara, Omari Issa alipokuwa akitoa mada kwa watendaji waandamizi wa Serikali.
 
Katika semina hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, Mawaziri, Makatibu Wakuu na viongozi wengine waandamizi wa Serikali, Bw. Issa alieleza uzoefu wa mwaka mmoja wa utekelezaji wa BRN Tanzania Bara.
 
Bw. Issa alisema mafanikio ya BRN kwa Tanzania Baya yametokana na nidhamu ya utendaji ambayo mfumo huo umeileta ikiwemo kuweka vipaumbele vichache vinavyogusa sekta muhimu kwa Taifa, kuweka muda na mfumo wa utekelezaji ili kupata matokeo ya haraka.
 
Akizungumzia mafanikio katika baadhi ya sekta yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa BRN Tanzania Bara, Bw. Issa alisema mpango huo umewapatia huduma ya maji wananchi milioni 2.3 ikiwa ni takribani mara tano zaidi ya kiasi ambacho Serikali ilikuwa ikikifikia kwa mwaka kabla ya mfumo huo.
 
Katika sekta ya uchukuzi, alisema mageuzi katika kuweka ufanisi kwenye bandari ya Dar es Salaam yameifanya bandari hiyo kuvuka lengo la BRN la kuhudumia mizigo tani milioni 13 mwaka kwa kufikisha kufikisha tani milioni 14 katika mwaka 2013/14 huku bandari hiyo ikianza kufanyakazi kwa saa 24, siku saba kwa wiki.
 
Akizungumzia sekta ya nishati alisema kaya zipatazo 193,000 zimeunganishwa na huduma ya umeme tangu Julai, 2013 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10. Mafanikio katika utekelezaji wa sekta sita za awali yameifanya Serikali kuingiza sekta mpya mbili za afya na uboreshaji wa mazingira ya biashara katika mfumo wa BRN ili nazo zipate ufanisi na zimeanza kutekelezwa.
 
Kwa upande wake mtaalamu ambaye pia ni Waziri Katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia na Mkuu wa Kitengo cha Utekelezaji wa Miradi ya Kipaumbele nchini humo (PEMANDU), Dk. Idris Jalla alisema Serikali nyingi duniani zina mipango mingi mizuri lakini utekelezaji ndio tatizo.
 
“Serikali nyingi duniani zina mipango na ahadi nzuri. Hata hivyo changamoto kubwa ipo katika kushindwa kuitekeleza,” alisema Bw. Jalla. Serikali ya Zanzibar ipo katika tafakuri ya kuutumia mfumo wa BRN ili kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka.