BRN Yapongezwa kwa Kuwasaidia Wakulima Wadogo

Yaya Olanirani

Yaya Olanirani

Na Mwandishi Wetu

MPANGO wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umepongezwa kwa kuweka katika moja ya sekta zake za kipaumbele, miradi ya kilimo inayolenga kuwasaidia wakulima wadogo nchini.
 
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Mwakilishi wa Rais wa Mpango wa UN wa Kusaidia Uwekezaji katika Kilimo (IFAD), Yaya Olanirani, wakati ujumbe wa taasisi hiyo ulipokutana na watendaji mbalimbali wa Serikali. IFAD ni asasi ya Umoja wa Mataifa inayosaidia uwekezaji katika kilimo.
 
“Tumefurahishwa na miradi ya BRN inayolenga katika kuwasaidia wakulima wadogo si tu katika jitihada za kuwaondolea umaskini bali pia kujiongezea kipato na kuwawezesha kupata utajiri.
 
“IFAD iko katika kufanya tathmini ya maeneo gani zaidi ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika siku zijazo lakini kwa sasa tutaendelea kusaidia juhudi za uwekezaji katika miundombinu ya kilimo na hasa eneo la kuwainua wakulima wadogo,” alisema.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais-Usimamizi wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayoratibu Mpango wa BRN hapa nchini, Bw. Omari Issa aliueleza ujumbe huo kuwa kupitia BRN Serikali ya Tanzania imedhamiria chini ya mfumo maalum wa usimamizi kuondoa changamoto za wakulima wadogo.
 
Akiwasilisha mada katika kikao hicho Mkurugenzi wa Sekta za Kilimo katika PDB, Bw. Henry Kinyuah alisema katika moja ya miradi ya mfano inayosimamiwa chini ya BRN ni shamba jipya la miwa lililopo Bagamoyo.
 
“Mradi wa uzalishaji wa miwa Bagamoyo peke yake utazalisha tani 150,000 za sukari kwa mwaka, makapi yatatumika kuzalisha mafuta, utazalisha umeme megawati 32, utazalisha ajira za moja kwa moja 2,300 na pia utawawezesha wazalishaji wadogo wadogo kuzalisha kati ya tani 300-400 za sukari,” alisema.