BRN Yaja na Mwarobaini Changamoto za Masoko ya Kilimo

Mtendaji Mkuu wa PDB Bw. Omari Issa akielezeaumuhimu wa sekta ya Afya kuingia BRN kuungana na sekta nyingine zilizotangulia zinazoendelea kuzaa matunda.

Mtendaji Mkuu wa PDB Bw. Omari Issa akielezeaumuhimu wa sekta ya Afya kuingia BRN kuungana na sekta nyingine zilizotangulia zinazoendelea kuzaa matunda.


Na Mwandishi Wetu

OFISI ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), imealika wataalamu wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora nchi inavyoweza kutatua changamoto ya masoko kwa wakulima.

Ili kufikia lengo hilo, maabara ndogo ya siku tano imeandaliwa ili kutathmini mifumo ya sasa ya masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga. Akifungua maabara hiyo jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa amewataka wadau wote husika kufanya kazi hiyo kwa pamoja katika kuleta majibu yanayolenga mikakati ya muda mfupi na mrefu ili kuwapatia nafuu wakulima.

“Nidhamu ya kiutendaji ya BRN inawataka wadau wa sekta za umma na binafsi kufanyakazi kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazozikabili sekta muhimu; ikiwemo ya kilimo,” alisema Bw. Issa na kuongeza kuwa majibu ya changamoto za masoko kwa wakulima yatakoka kwenye pande pande hizo mbili.

Maabara hiyo ndogo inajumuisha wawakilishi 50 kutoka sekta za umma, binafsi, taasisi za kimataifa na wakulima wenyewe. Tanzania nzima, na hususani miradi ya kipaumbele ya kilimo iliyo chini ya BRN, ilishuhudia uzalishaji mkubwa wa mahindi na mpunga katika msimu wa 2013/14; jambo ambalo limeleta fursa nzuri lakini pia lilikuja na changamoto zake.

Kwa mfano katika msimu huo, uzalishaji wa mahindi ulifikia tani milioni 6 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani milioni 4.5 kwa wastani katika miaka mitano ya nyuma. Mpunga ulifikia tani milioni 1.7 kutoka tani milioni 0.85 mwaka uliotangulia.

Mwisho wa maabara hii, washiriki wataibua mapendekezo na mpango wa utekelezaji utakaoainisha mfumo madhubuti wa masoko ya mahindi na mpunga. Inatarajiwa kwamba mapendekezo haya yataweza kutumika kwa mazao mengine pia.

BRN ni mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ulioasisiwa na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha nchi inapata mafanikio makubwa nay a haraka katika sekta sita za kipaumbele ambazo ni elimu, kilimo, maji, nishati, uchukuzi na ukusanyaji wa raslimali.