Na Hassan Abbas
MPANGO wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaosimamiwa na Kitengo cha Rais cha Utekelezaji wa Miradi Mikubwa (PDB), umeendelea kupata mafanikio katika kuhakikisha mapinduzi ya kilimo nchini.
Akitoa mada jana (Alhamisi) Dar es Salaam katika mkutano wa siku tatu unaohusisha wadau wa sekta ya kilimo kutoka nchi mbalimbali, Naibu Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Peniel Lyimo alisema tayari BRN imeanza kuonesha mafanikio katika maeneo yote ikiwemo kilimo.
“Kutokana na umuhimu wake katika kuchangia maendeleo ya Taifa sekta ya kilimo ilichaguliwa na wataalamu na kuidhinishwa na Serikali kuwa moja ya maeneo sita ya kipaumbele katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
“Tayari tumeanza kuona matokeo Makubwa katika maeneo ambayo BRN imeyaainisha ili yapewe fedha za kutosha kwa lengo la kuboresha kilimo chetu kuwa cha kisasa na chenye tija katika maisha ya mkulima mwenyewe,” alisema Bw. Lyimo.
Akitoa takwimu mbalimbali kuhusu mafanikio ya BRN katika sekta ya kilimo, Bw. Lyimo aliongeza kuwa tayari kampuni za kuendesha mashamba ya kisasa ya wakulima zimeanza kusajiliwa ili kuchagiza kilimo cha kisasa na maghala maalum kwa ajili ya kuhifadhi mazao yameshaanza kujengwa.
“BRN imelenga kuchagiza mapinduzi ya kilimo katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa ya mwaka 2025,” alisema na kuwataka wadau wote kushirikiana na Serikali katika kutekeleza na kufikia malengo hayo.
BRN ni mfumo wa utekelezaji wa miradi ya vipaumbele ambao Serikali imeanza kutekeleza tangu mwaka 2013 kwa kuunda Kitengo Maalum cha PDB kuhakikisha kuwa wizara husika zinatekeleza malengo yaliyowekwa kwa wakati na viwango. Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi mikubwa itakayokamilika katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 BRN imejikita katika sekta sita ambazo ni kilimo, nishati, maji, usafirishaji, elimu na raslimali fedha.