TAARIFA ambazo mtandao huu umezipata muda si mrefu ni kwamba kikao cha majadiliano cha madaktari kilichokuwa kikifanyika leo Ukumbi wa Water Front (NSSF) kimemalizika na madaktari hao wametoka na maazimio ya kurudi kwenye mgomo kuanzia Jumatano hii (Machi 7, 2012).
Kwa mujibu wa taarifa ambayo wameitoa ni kwamba wamefikia uamuzi huo baada ya kuona makubaliano ambayo Serikali iliahidi kuyafanyia kazi hayajatekelezwa kwa kiwango kilichotarajiwa.
Wamesema wanaamini kikwanzo cha maridhiano yao ni Serikali kushindwa kuwang’oa madarakani Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda pamoja na Naibu Waziri wake, jambo ambalo halijafanyiwa kazi hadi sasa.
Kikao hicho kimetoa muda hadi Jumatano na kuitaka Serikali (ngazi za juu) kutoa tamko la utekelezaji wa suala hilo na kama itafika siku hiyo kukiwa hakuna tamko lolote madaktari hao watarudi kwenye mgomo nchi nzima.
Miongoni mwa madai ambayo madaktari awali walitaka yafanyiwe kazi ni pamoja na Serikali kuwaondoa madarakani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akilishughulikia suala hilo amemsimamisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na kuvipa kazi vyombo vya dola kufanya uchunguzi kama kulikuwa na uzembe wowote juu ya suala hilo. Mtandao huu utatoa taarifa zaidi ya habari hii mara baada ya kukamilisha.