Breaking Newz: Watuhumiwa wanne wakutwa na hatia

Mmoja wa watuhumiwa wa kesi hiyo, Uhuru Kenyatta


MAHAKAMA ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya The Hague, Uholanzi, imewatia hatiani watuhumiwa wanne kati ya sita wa Kenya wanaotuhumiwa na ghasia zilizoikumba nchi hiyo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Taarifa ambazo mtandao huu umezipata mchana huu watuhumiwa hao sasa watakuwa na kesi ya kujibu kuhusiana tuhuma zinazowakabili. Hata hivyo bado majaji hawajaweka hadharani majina yao. Majina hayo yatawekwa hadharani muda si mrefu kuanzia sasa.

Mtandao huu utakupa taarifa hapo utakapozipata. Watuhumiwa sita wanaokabiliwa na makosa hayo tangu awali ni Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto, Waziri wa Viwanda, Henry Kosgey, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura, aliyekuwa Mkuu wa Polisi, Generali Hussein Ali na Mtangazaji wa Redio, Joshua Arap Sang.

Taarifa kutoka ICC, inasema jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Ekaterina Trendafilova linawasilisha uamuzi wao muda huu kwa watuhumiwa na mawakili wao kwanza kupitia maandishi, na baadaye majina ya waliokutwa na hatia yatawekwa hadharani.

Kiongozi wa mashtaka katika ICC, Luis Moreno Ocampo anadai kwamba Kenyatta na wenzake walifadhili na kutekeleza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa chama cha Orange Democratic Party, ODM, chake Waziri Mkuu, Raila Odinga, katika maeneo ya Nakuru na Naivasha mkoani Rift Valley.

Watu wasiopungua 1,300 waliuwawa wakati wa ghasia hizo, na wengine zaidi ya 500,000 wakapoteza makazi. Ghasia zilizuka baada ya Rais Kibaki kutangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali kati yake na Odinga. Kufuatia ghasia hizo, jamii ya kimataifa iliwashinikiza, Kibaki na Odinga kufanya mazungumzo ili kuzimaliza.