BAADA ya Kamati ya Bunge Huduma za Jamii kumaliza kazi ya kufanya mazungumzo kati ya Serikali na madaktari walioko katika mgomo, imewasilisha taarifa yake bungeni jana jioni.
Akitoa taarifa fupi muda huu bungeni leo kwa niaba ya Kamati hiyo, Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amewaeleza wabunge baada ya kamati hiyo kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Uongozi jana usiku. Bunge, kupitia kwa Spika baada ya kujadiliana na kamati hiyo wamefanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kutoa maelekezo kulingana na hali halisi.
Bunge limesema mgogoro wa mawasiliano kati ya Wizara na Madaktari utachukuliwa hatua leo huku madai yao ya msingi na ya haraka yanashughulikiwa leo hii katika mazungumzo kati ya Waziri Mkuu na madaktari.
“…Kwanza tunaomba kwa dhati na Bunge hili linaomba madaktari warudi kazini leo, mawasiliano yaliokuwa kati ya wizara na wao yanachukuliwa hatua leo…madai yao yatatatuliwa Waziri Mkuu anazungumza sasa,” alisema Spika Makinda.
Amesisitiza kuwa hali ni mbaya hasa Muhimbili kwani wajumbe wa Kamati waliotembelea Hospitali hiyo baadhi wametoa machozi kutokana na hali ilivyo. Hivyo kuiomba Serikali kuhakikisha inamaliza mgogoro huo leo na hali kurejea ya awali. Amewata wabunge na vyombo vya habari kulifanya suala hilo kiushabiki kwani hali ni mbaya mahospitalini.