Breaking News; Kanisa Katoliki Lalipuliwa Arusha

KANISA Katoliki Parokia Teule ya Mt. Joseph Mfanyakazi Olasiti la jijini Arusha limelipuliwa na mlipuko unaodhaniwa kuwa ni bomu la kurushwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP, Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea majira ya saa tano asubuhi wakati watu wakiwa katika Ibada ya Ufunguzi wa Parokia hiyo teule ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi. Hadi sasa mtu mmoja anashikiliwa na polisi kutokana na tukio hilo ambapo inasemekana alirusha mlipuko huo akitokea nyuma ya umati wa waumini.

Kamanda Sabas alisema watu wapatao 30 wamejeruhiwa majeraha madogomadogo na wengine 3 wamejeruhiwa majeraha makubwa na ambapo mpaka sasa wanatibiwa katika hospitali za Mount Meru, Seriani na hospitali nyingine.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa amesema kuwa Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vinafanya kazi ili kugundua mlipuko huo ni wa aina gani na kuwataka watanzania wote kuwa watulivu na wenye usikivu ili kuifanya kazi hiyo kufanyika kwa ufasaha. Pia amewataka wakristo wote kuondoa hali ya wasiwasi na mashwari kwani vikosi hivyo vitatoa majibu ya uhakika.

Ibada hiyo iliyokuwa ya Uzinduzi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi ilikuwa ikiongozwa na Mhashamu askofu Josephat Leburu na Balozi wa Papa Fransisco Montesilo.