TAARIFA kutoka Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeeleza kuwa mashua moja iliyokuwa imebeba bidhaa na abiria imezama na karibu watu 36 wamefariki dunia. Maofisa wanasema kuwa zaidi ya watu 100 wamenusurika.
Inaripotiwa kuwa ajali hiyo ilitokea siku ya Jumatatu umbali wa kilomita 30 kutoka Mji wa Kisangani na kusababisa maandamano yaliyofanywa na vijana wenye hasira kwenye Mji wa Isangi ambapo mashua hiyo ilikuwa ikielekea. Nyumba kadha za Serikali zinaripotiwa kuchomwa na waandamanaji hao wenye hasira.
Wakati huo huo, Jeshi la kulinda Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia limesema askari wake watatu na kandarasi raia wameuawa katika shambulio lililofanyika katika makao yake makuu mjini Mogadishu. Taarifa ya Umoja wa Afrika imesema wapiganaji wa al-Shabab waliingia katika kambi wakivalia sare kama askari wa Jeshi la Serikali ya Somalia.
Taarifa hiyo imesema washambuliaji watano waliuawa na wengine kadha kukamatwa. Pamoja na kutoa eneo hilo kuwa makao makuu ya majeshi ya kulinda amani ya AU nchini Somalia, eneo hilo lililoimarishwa pia makao ya balozi za Uingereza na Italia.