Frank Mvungi- Maelezo, Bagamoyo
SERIKALI ya Tanzania imeahidi kuendelea kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa za Uchumi na fedha kwa wananchi ili kuongeza wigo wa wananchi kushiriki katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu. Hayo yamesemwa leo mjini Bagamoyo na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Juma Reli wakati akifungua Semina kwa waandishi wa habari za Uchumi na Fedha iliyoandalliwa na Benki hiyo.
Akifafanua, Reli amesema waandishi wa habari wanalo jukumu la msingi la kuuhabarisha umma kuhusu majukumu ya Benki hiyo katika kukuza uchumi na fursa zinazotolewa na Serikali ili kuwanufaisha wananchi.
“Navipongeza Vyombo vya habari hapa nchini kwa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za uchumi na fedha kwa wananchi” alisema Reli.
Akizungumzia Lengo la Semina hiyo Reli amesema imelenga kuwaongezea ujuzi na weledi waandishi hao ili kuwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo na namna wanavyoweza kunufaika nazo.
Naye Meneja Uhusiano na Itifaki wa BOT, Bi. Zalia Mbeo alisema kuwa mwaka huu waandishi wa habari wapatao 20 wanashiriki katika Semina hiyo ambapo mwaka jana ilifanyika kwa mara ya kwanza na ilihusisha waandishi wa habari 15.
Pia bi Mbeo alisema BOT itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari hapa nchini kwa kuwa ni wadau muhimu katika kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu Kazi zinazotekelezwa na Benki hiyo kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.
Mada zitakazotolewa katika Semina hiyo ni pamoja na Ushiriki wa wananchi katika dhamana za Serikali, Soko la pamoja kwa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki, Kurugenzi ya uchumi na Sera, Kurugenzi ya huduma za Kibenki na Sarafu, Kurugenzi ya usimamizi wa Mabenki, Kurugenzi ya Mifumo ya malipo na Bodi ya Bima ya Amana.