Na Mwandishi Wetu, Los Angeles, CA
ILE siku ya Septemba 3, ambayo ilikuwa ikisubiriwa na wa-Afrika wengi hapa jijini Los Angeles iliwadia. Timu 24 za mataifa ya Kiafrika zilikutana kwa ajili ya kuchuana kwenye mpira wa miguu, ambao mshindi alijinyakulia donge nono la Dola 3000! Timu ya Watanzania ‘Bongo Starz’ ya jijini Los Angeles iliweza kuichapa Ivory Coast bao 4 kwa 1 bila matatizo yeyoye katika duru la kwanza la mashindano hayo.
Bongo Starz haikupewa nafasi kubwa sana katika mashindano hayo kutokana na ugeni wake kwenye mashindano ukilinganisha na timu za Nigeria, Cameroon na Ghana, ambazo zina uzoefu mkubwa na hazina kubwa ya wachezaji. Ushindi mnono wa Bongo Starz uliwawezesha kwenda duru la pili na kukutana na kigingi cha Ghana. Ghana ilifanikiwa kuichapa Bongo Starz bao 1 kwa mtungi, na hivyo basi Bongo Starz kutolewa katika mashindano hayo. Pamoja na hayo Ghana haikuweza kuchukua Kombe baada ya kupigwa mueleka na vijana wa Sierra Leonne, ambao ndio waliibuka washindi katika mashindano hayo.
Mashindano hayo yalifanyika kwa siku moja tu (Tournament) kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa mbili usiku, na yaliambatana na mauzo ya bidhaa mbalimbali, muziki, na mapochopocho kutoka nchi husika. Kwa picha zaidi za mashindano haya, tembelea ukurasa wetu wa MATUKIO KATIKA PICHA, kwa kubofya hapa: http://www.thehabari.com/matukio/bongo-starz-yaichapa-ivory-coast-bao-4-kwa-1-2
(Picha zote na Abdul Majid)