BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini na machachali ulingoni, Zumba Kukwe “Chenji dola” anatarajia kupanda ulingoni Alhamisi Novemba 27, 2014 kuzipiga na bondia mkongwe, Sweet Kalulu katika ukumbi wa Kontena uliopo Kibaha Maili Moja. Taarifa zinasema mabondia hao watacheza pambano la raundi nane, lisilo la ubingwa na mshindi kati yao atacheza na mshindi kati ya mabondia, Thomas Mashali na Dula Mbabe watakaopambana Decemba, 2014.
Akilizunguzia pambano hilo kwa wanahabari kiongozi wa ngumi za kulipwa na Mratibu wa pambano alisema maandalizi yanakwenda vema chini ya udhamini wa George Nyasulu aliependekeza mchezo upigwe Kibaha Maili Moja alipotokea Zumba Kukwe na kutanua wigo wa masumbwi nchini.
Alisema hamasa hiyo itachangia mchezo wa ngumi kuchezwa kila kona ya nchi na sio kila siku mabondia kucheza Jijini Dar es Salaam tu, huku watu wa mkoa wa pwani nao wapate nafasi ya kuwaona vijana wao wanaotikisa mjini kwani Kibaha kuna mabondia wengi wazuri na wakali ambao hawajawahi cheza kwao.
Hivyo katika mapambano ya utangulizi kutakuwepo na mabondia wote wakali wa Mkoa wa Pwani wakicheza na wenzao toka sehemu mbalimbali za jiji kama vile Mustafa Doto atazipiga na Ramadhan Max, huku Shadrack Ignas akioneshana kazi na Fredy Masinde, naye ‘Dogo Janja’ Issa Omar Nampepeche atazipiga na Rajabu Miafro na mapambano mengine mengi ya utangulizi.
Alisema waandaaji wamepanga kuweka kiingilio kidogo ili kuwawezesha watu wengi kuja kushuhudia pambano hilo la aina yake ambalo si la kukosa.