Na Mwandishi Wetu
BINGWA wa mkanda unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Abdalah Mohamed ‘Prins Naseem’ atapanda ulingoni Februari 24 kutetea mkanda wake kwa kuzichapa na bondia Salehe Mkalekwa. Pambano hilo la ubingwa wa PST litakuwa na uzito wa kg 57
na litashirikisha mapambano mengine manne ya utangulizi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa pambano hilo Shaban Adiosi ‘Mwayamwaya’ alisema pambano litafanyika katika Ukumbi wa New Kibeta uliopo Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam.
Alisema pambano hilo la ubingwa wa PST ni muendelezo wa shirikisho
hilo kuendelea kuwainua mabondia chipkizi ambao hawajawa na majina
makubwa ili nao waweze kufikia kiwango kizuri cha mchezo huo.
“Ubingwa huu wa PST ni maalum kwa ajili ya mabondia chipkizi na ndio
maana mabondia wanaoshirikishwa wengi ni chipukizi na lengo ni
kuendeleza vipaji vyao,” alisema Mwayamwaya.
Aliyataja mapambano ya utangulizi yatakayopamba pambano hilo yatakuwa kati ya Shaaban Zungu na Hasan Salehe watakaopigana uzito wa kg 55, Safari Mbeyu na Ibrahim Maokola watakaopigana uzito wa kg 67, Jofrey Pacho atakayetwangana na Seleman Shaaban na Abdalah Yusuph atakayepigana na Omari Kijepa.
Mbali na kuwepo mapambano ya ngumi kutakuwa na uuzwaji wa DVD zenye mapambano ya mabingwa wa dunia akiwemo Manny Paquaio, Floyd Maywherth, Roy Jones na wengine kibao ‘DVD’ hizo zilizoandaliwa kwa ubora wa hali ya juu zitakuwa zikiuzwa kwenye mpambano huo na Kocha Rajabu Mhamila ‘Super ‘D’.
“Ninatarajia kuwapelekea DVD mashabiki wa ngumi watakaokuwepo katika pambano kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sheria za mchezo wa ngumi,” alisema Super ‘D’.