MTANZANIA Fadhili Majia sasa atamvaa Mghana Isaac Quaye tarehe 8 March kutafuta nafasi ya kugombea mkanda wa ubingwa wa Jumuiya ya madola (CBC) ambayo unashikiliwa na bondia Kevin Satchell wa Uingereza.
Mpambano wa Majia na Quaye umemsogezwa mbele kwa kuwa mashindano ya ubingwa wa Afrika yanayoendelea nchini Afrika ya Kusini yanarushwa na televisheni ya Super Sports ambayo ndio wafadhili wakubwa wa mpambano wao.
Wakati huo huo bondia Richard Commey wa Ghana atamvaa Mghana mwenzake Bilal Muhammed kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati uzito wa lightweight siku hiyo hiyo March 30.
Aidha bondia Frederick Lawson wa Ghana atazichapa na bondia Isaac Sowah wa Ghana kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika uzito wa Welterweight. Mapambano hayo yatasimamiwa na Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi
Mtanzania mwingine atakaye peperusha bendera ya taifa siku hiyo ni pamoja na Allan Kamote atakayezichapa na bingwa wa zamani wa IBF wa mabara na ambaye ndiye bingwa wa sasa wa WBA wa mabara Emmanuel Tagoe katika pambano lisilo la ubingwa.
Naye bondia wa Kenya Michael Odhiambo atachuana vikali na Mghana George Ashire katika mpambano usio wa ubingwa uzito wa lightweight.
Mapambano hayo yote yatakuwa ni ya utangulizi katika mpambano wa ubingwa wa dunia kati ya bondia maarufu wa Ghana anayeishi nchini Marekani Joseph Agbeko na Luis Mendelez kutoka nchini Columbia. IBF/Afrika inawaomba watanzania kwa ujumla wao wawaombee mabondia wake ili waweze kupeperusha vyema bendera ya taifa.
Wakati huo huo; RAIS wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa IBF bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, Mtanzania Onesmo Ngowi atakuwa msimamizi mkuu wa mapambano ya ubingwa wa yatakayofanyika nchini Ghana tarehe 8 na 30 March 2013.
Mapambano hayo ni yale yanayowakutanisha mabondia Richard Commey akipambana na Mgana mwenzake Bilal Mohammed wakigombea mkanda wa IBF Afrika na Ghuba ya Uajemi (IBF AMEPG) katika uzito wa Lightweight. Mabondia wote wawili wana rekodi zinazovutia, Commey ana makazi yake katika jiji la London nchini Uingereza.
Mpambano wa pili siku hiyo utawakutanisha mabondia wawili wa Ghana Fredrick Lawson akipambana na bondia machachari Isaac Sowah. Wote wanaishi nchini Ghana. Mapambano yote yatafanyika wakati bingwa wa dunia wa zamani wa IBF Joseph Agbeko atakapochuana na bondia Luis Melendez wa Mexico kugombea ubingwa wa dunia wa IBO katika uzito wa bantam.
Mpambano mwingine ambao Ngowi atasimamia ni kati ya bondia Helen Joseph wa Nigeria na Fatuma Zarika wa Kenya ambao watagombea mkanda wa IBF wa mabara wa wanawake. Helen Joseph ni mkazi wa Ghana wakati Fatuma Zarika anaishi nchini Ujerumani.
Maofisa wengine watakaomsaidia Ngowi katika mapambano hayo ni pamoja na: Refarii: Rodger Barnor, Jaji namba 1 ni Fred Ghartey, Ghana, Jaji namba 2 ni Confidence Hiagbe na jaji namba 3 ni May Mensah Akakpo, Ghana. Mapambano haya ni kati ya mapambano 100 ambayo IBF imepania kuyafanya katika ukanda wa Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati mwaka huu 2013.