BONDIA Jafet Kaseba wa Tanzania amemshinda bondia Rasco Chimwanza wa kutoka Malawi katika pambano la ubingwa lililofanyika Ukumbi wa DDC Magomeni Kondoa, ukumbi ambao kwa sasa umesahaulika na kuwa katika hali mbaya ya kiuchakavu.
Kaseba ameshinda mpinzani wake kwa TKO katika ’round’ ya sita baada ya M-malawi Chimwanza kushindwa kuendelea kufuatia makonde mfululizo aliyotupiwa na mpinzani wake, ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi na kucheza chini ya kiwango kilichotarajiwa.
Kabla Jafet Kaseba hajatoana jasho na mpinzani wake kulikuwepo na mapambano zaidi ya nane ya utangulizi ambayo yalikuwa makali na kusisimua, kati ya hayo ni bondia mdogo Issa Omar alitwangana na mkongwe Juma Seleman katika pambano lililokuwa na mvuto na kuwafanya watu muda wote washindwe kukaa katika viti.
Omar alimshinda mkongwe huyo, pambano lingine Juma Fundi alimsambaratisha Moro Best kwa kichapo kikali, huku Kamanda wa Makamanda alishindwa vibaya na Ibrahim Maokola. Mgeni mwalikwa wa pambano hilo mamaa Dotnata alimvisha kaseba mkanda wa ubingwa na kuahidi kuandaa pambano la ngumi kwa siku zijazo na hasa kati ya Alphonce Mchumiatumbo na Iddi Bonge.