Na Mwandishi Wetu
BONDIA maarufu nchini Tanzania, Francis Cheka anatarajia kupanda uringoni kuvaana na bondia Udiadia Mwahia kutoka nchini DRC Kongo ikiwa ni pambano la kugombea mkanda wa Ubingwa wa IBF barani Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi.
Mabondia hao wanatarajia kukutana katika mpambano wa kwanza tangu Mkoa wa Arusha kutangazwa Jiji na pambano lao linatarajia kufanyika katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Desemba 26, 2012 siku ya Boxing Day.
Akimtambulisha Francis Cheka kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa Melezo jijini Dar-Es-Salaam leo, mratibu wa mpambano huo na ambaye alishawahi kuwa bingwa wa Tanzania kwenye ngumi za ridhaa George Andrew alisema kuwa bondia Udiadia Mwahila anakaa Lusaka Zambia ambako ndipo anapofanya shughuli zake za ngumi chini ya promota maarufu Anthony Mwamba!
Udiadia ana rekodi ya mapambano 12 na ametoka sare pambano moja na hajapoteza hata moja wakati Francis Cheka ana rekodi ya mapambano 33 amepoteza 6 na kutoka sare pambano moja.
George alisema kuwa mpambano huo utatumika kulitangaza Jiji la Arusha kama Las Vegas ya ngumi katika bara la Afrika na kulifananisha Jiji la Arusha na Jiji la Geneva lililoko nchini Switzerland.
Mpambano huo unakuja wakati ambapo mpambano mwingine wa Francis Cheka na bondia kutoka Ujerumani wa kugombea mkanda wa IBF wa mabara ulifutwa baada ya Simon kuumia katika mazoezi.
Naye Rais wa IBF katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Ghuba ya Uajemi Onesmo Nhowi alisema kuwa wao kama IBF wamesharuhusu maandalizi ya mpambano huo. Rais huyo aliwataka wadhamini pamoja na wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa mingine kujitokeza kwa wingi ili kulifanya pambano hilo kuwa la mafanikio.
Naye bondia Francis Cheka alisema kuwa amejiandaa kwa kiasi kikubwa na atazidi kufanya mazoezi ili kupata ushindi kwake pamoja na nchi ya Tanzania. Aliendelea kusema kuwa kila Mtanzania anajua uwezo wake kwa hiyo amewataka wote wafike kwa wingi ili kupata uhondo na burudani tosha!