Na Mwandishi Wetu
BONDIA wa uzito wa ‘Bantamweight’, Fadhili Majiha ‘Stoper’ mwishoni mwa wiki alikuwa na kibarua kizito kutoka kwa bondia wa Thailand, Pungluang Sor Singyu aliyemenyana naye nyumbani kwao Thailand na kupigwa kwa pointi.
Akizungumzia matokeo hayo, Stoper amejinasibu kuwa alipaswa kushinda pambano hilo kwani alicheza kwa umakini mkubwa lakini waamuzi walimpendelea mpinzani wake kwa kuwa alikuwa akicheza nyumbani. “…Kacheza kwao na mcheza kwao utunzwa…maana nilicheza kwa ustadi wa hali ya juu na wapenzi wote wa ngumi walikuwa upande wangu lakini nilinyimwa ushindi,” alisema Majiha.
Bondia huyo ambaye anatamba nchini kuwa hakuna bondia anaeweza kumpiga na anadai mara zote anaopangiwa nao wamekuwa wakimkacha ameonya yeyote atakayejitokeza atatoa dozi kuweka heshima na historia. “…Mabondia Fransic Miyeyusho pamoja na Nassibu Ramadhani nawapa onyo, ole wake atakayeingia anga zangu atakiona cha moto, hawa mechi zao nyingi wanapenda kupangiana wenyewe kwa wenyewe,” alisema.
“Nimerudi nyumbani nipo fiti sina hata kovu la aina yoyote, hivyo nitahakikisha nafanya mazoezi kujiweka fiti zaidi, napenda kutoa tahadhali kwa bondia yoyote Mtanzania atakayejitokeza kwa sasa mbele yangu yeye atakuwa halali yangu,” alisema Majiha.
Naye kocha wa bondia huyo, Waziri Chara amejigamba kuwa bondia wake ni wa kimataifa kwani michezo yake karibia mitatu kacheza Philippines na mwingine Thailand hivyo wao ni wa kimataifa zaidi na mapambano waliocheza nje yote yalikuwa magumu na ya raundi 12 ambapo zote bondia wake alimaliza.