BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini Abdallah Paziwapazi a.k.a ‘Kiroba’ au kama anavyojulikana na wengi ‘Dula Mbabe’ anatarajiwa kupanda ulingoni Juni 29, 2014 katika Ukumbi wa CCM Mwinjuma, Mwananyamala jijini Dar es Salaam kuzipiga na Hamis Juma ambaye ameonekana mbadala wa bondia Maneno Osward.
Mpambano huo ambao utakuwa wa vunja jungu yaani wa kukaribisha mwezi mtukufu wa ramadhani, utaambatana na mapambano mengi ya utangulizi yakiwemo mawili ya kumaliza uhasama wa wababe wa kitaa, yaani mbabe wa Mwananyamala kwa Mama Zakaria, Mwinyi Mzengera ‘mambwa’ na mbabe wa Mwananyamala kwa Kopa, George Manywele ‘G-Mawe’.
Kwa upande wake mbabe wa Mwananyamala Kisiwani, Joseph Peter “Mbowe” atazipiga na Zumba Kukwe, huku kukiwa na pambano kali la vijana wanaocheza ngumi, akiwemo Issa Omar Nampepeche ‘peche boy’ atakaye zipiga na Ramadhani Kumbele katika pambano la raundi nane, pambano hili linategemewa kuwa zuri kutokana na mabondia wote kuwa machachari wanapokuwa ulingoni.
Ukiachilia mapambano haya yenye vibweka pia kutakuwepo na mapambano mengine ya utangulizi kama vile yule mwimbaji maarufu wa mapacha watatu Khareed Chokolaa atakapozipiga na Daud Giligili, huku chidi mbishi kumvaa Ramadhan Hamis, Dj Kulwa atazipiga na Alex Kado na Masango Komakoma ataminyana na Mohamed Amir ‘alkaida.’
Mapambano yote yameandaliwa na Bigright Promotion, chini ya kiongozi wake Ibrahim Kamwe ambaye siku zote amejitahidi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mchezo wa bondia unakuwa ajira kwa vijana na inachezwa mara kwa mara kujenga ufanisi zaidi.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kamwe alisema maandalizi kwa kiasi kikubwa yamekamilika na mabondia wapo katika hali nzuri ya ushindani na kuwasihi watu wajitokeze kuangalia ngumi kali zenye ushindani, ukizingatia kuwa ukumbi umekarabatiwa na kila mtu atakaa katika kiti chake na ulinzi mkali utakuwepo ili kuboresha mchezo wa ngumi usiwe sehemu ya mchezo wa fujo na kila atakaekuja kwa nia ya kufanya fujo atachukuliwa hatua kali za kisheria.