MTU mmoja amejeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Ziwa Victoria, Makongoro Misheni, Mwanza.
Aliyejeruhiwa ni mhudumu wa nyumba ya wageni ya kanisa hilo, Benadeta Alfred (25) aliyekumbwa na mkasa huo juzi saa mbili usiku. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema jana kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ni bomu la kutengenezwa kienyeji linalojulikana kwa jina la IED na kwamba uchunguzi unaendelea kuwabaini walioliweka kanisani.
Mlowola alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa polisi wanapoona vitu ambavyo wanavitilia shaka ili uchunguzi wa kitaalamu ufanyike kabla ya kusababisha madhara. Mlinzi wa kanisa hilo, Charles Mathayo alisema walisikia kishindo kikubwa cha mlipuko na baada ya muda mfupi wakasikia kelele za mhudumu huyo akiomba msaada.
Alisema walipofika eneo la tukio, walimkuta akiwa ameanguka huku akitokwa damu sehemu mbalimbali za mwili pembeni mwake kukiwa na vitu ambavyo alisema hakuvifahamu. Shuhuda mwingine, mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta kanisani hapo, Erina Emmanuel alisema walisikia mlipuko, baadaye wakasikia sauti ya mtu akiomba msaada, lakini kutokana na hofu walikimbia hawakwenda kumsaidia.
Lilifungwa kama zawadi
Kiongozi mmoja kanisani hapo ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kitu hicho kilicholipuka kilikuwapo kanisani hapo tangu Ijumaa iliyopita, kikiwa kimewekwa juu ya makreti ya soda. Alisema wahudumu walipuuza wakidhani ni mzigo wa mtu aliyekuwa ameusahau kutokana na jinsi ulivyokuwa umefungwa vizuri kwa karatasi za zawadi.
Alisema baada ya kuona bahasha hiyo imekaa muda mrefu bila kuchukuliwa, mhudumu huyo aliichukua kwa lengo la kuipeleka kwa uongozi wa kanisa. Alipoushika, mzigo huo ulilipuka na kumjeruhi usoni na miguuni na kupelekwa Hospitali ya Bugando ambako amelazwa.
Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Bugando uliwazuia waandishi wa habari kumwona majeruhi huyo.