Boko Haram Wauwa Wanafunzi 25 wa Chuo Nigeria

Anayedaiwa kuwakiongozi wa Kundi la Boko Haram

ZAIDI ya wanafunzi 25 wa Chuo cha Ufundi Mubi wameuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Mubi, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. Taarifa za Polisi nchini Nigeria zinasema kuwa shambulizi hilo limetokea katika mabweni ya chuo hicho yaliopo mbali kidogo na chuo chenyewe kinachotoa mafunzo ya ufundi anuwai mjini Mubi.
Hata hivyo taarifa zilizotolewa na mhadhiri mmoja wa chuo hicho zinaeleza kuwa wanafunzi waliokuwa wanafikia 40, lakini bado taarifa hizo hazijathibitishwa. Mauaji haya yanakuja siku chache baada ya operesheni kali kufanywa dhidi ya kundi la wapiganaji wa Kiisilamu la Boko Haram mjini humo.

Aidha taarifa zaidi kutoka kwa mhadhiri mmoja wa chuo hicho ambaye hakutaka kutaja jina lake, wanafunzi hao kabla ya kuuwawa waliamrishwa kupanga foleni na kutaja majina yao mmoja baada ya mwingine kisha kuuawa. Haijulikani kwa nini baadhi waliuawa na wengine kuachwa, baadhi ya waliouawa pia wamo Waislamu. “Kila mtu anaogopa na wamejifungia vyumbani,” alisema mhadhiri huyo.

Aliongeza kuwa wanafunzi sasa wameanza kuuhama mji huo. Inasemekana wameweka majani ya rangi ya kijani kibichi kwenye magari yao kama ishara kuwa hawaungi mkono upande wowote. Wapiganaji wa Boko Haram wanaopigana wakitaka sheria za kiisilamu kutumika, wamewaua zaidi ya watu 1,000 Kaskazini mwa Nigeria.

-BBC

Majeshi ya Kenya Yatangaza rasmi Kuutwaa Mji wa Kismayu

JESHI la Kenya limetangaza kuwa Mji wa Bandari wa Kismayu uliokuwa ukitawaliwa na Al-Shabaab kwa hivi sasa unadhibitiwa na majeshi ya Umoja wa Afrika pamoja na Somalia (AMISOM) baada ya jitihada zao zilizodumu kwa siku kadhaa.

Msemaji wa Jeshi la Kenya katika operesheni hiyo Emanuel Chirchir amesema kwa njia ya simu kwamba majeshi ya Umoja wa Afrika na yale ya Somalia yameuzunguka mji wa Kismayu na pia kuidhibiti bandari ya mji huo wa kusini. Chirchir amesema wakati majeshi hayo yakiingia mji wa Kismayuu, watu walitoka nje ya nyumba zao na kushangilia kwa kupiga makofi kuonesha kuunga mkono hatua hiyo.

Akijibu suala iwapo majeshi hayo yatafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwakamata al-Shabaab, Chirchir alisema wakaazi wa Kismayuu wengi wanajishughulisha na biashara na kwamba hawaoni haja ya kuingia kwenye nyumba kufanya msako kama huo.

Alisema wanajeshi wa majeshi ya Afrika na Somalia waliokuwa Kaskazini Magharibi mwa mji waliingia bila ya purukushani zozote ndani ya mji na wanaelekea uwanja wa ndege ambapo kwa sasa hakuna matukio ya mashambulizi kwenye mji wa Kismayu na kwamba mji umetulia kabisa.

Akieleza kama anafahamu wapi Al shabab wamekimbilia kwa sasa Chirchir alisema wanadhani wanamgambo hao wapo katika eneo la Barawe na kwamba vikosi vya Jeshi la Umoja wa Afrika na Somalia vitafika huko. Alisema zipo taarifa kuwa wanamgambo hao wanataka kujisalilimisha, nao wametoa wito kwa wanamgambo hao kufanya hivyo.

Siku ya Jumatatu kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni al-Shabaab walirusha kombora kwenye kituo cha polisi cha Garissa kilicho karibu na mpaka wa Somalia,ambapo siku moja kabla polisi wawili waliuawa baada ya kushambuliwa kwa risasi katika mji huo.

Mkuu wa Wilaya ya Garissa Mohammed Maalim alisema kombora la kurushwa kwa mkono liliripuka lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa na mashambulizi ya silaha kati ya kundi la Alshabab na yale ya Afrika na Somalia yaliweza kudumu kwa muda wa dakika kumi wiki iliyopita. Kuondoshwa kwa wanamgambo wa kundi la al-Shabaab mjini Kismayu inaweza kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha usalama katika eneo hilo ambalo limekuwa mara kadhaa katika vita isiyokwisha.

Kwa upande wake Marekani imeyapongeza majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Kenya kwa kulikimbiza kundi la al-Shabaab nchini Somalia katika bandari ya Kismayu na kuwataka viongozi wa Somalia kudumisha usalama katika bandari hiyo.

Mwanadiplomasia wa Marekani Barani Afrika Johnnie Carson aliwaelewa waandishi wa habari akiashiria katiba mpya ,bunge jipya na rais mpya wa Somalia kwamba Somalia ipo katika historia mpya baada ya miaka mingi ya ugoigoi.

Umoja wa Afrika wenye majeshi 17,000 nchini Somalia waliingia mji wa Kismayu siku ya Jumatatu na kuanza kuwafurusha nje ya mji huo wanakikundi cha al- Shabaab. Marekani pia inaweka kipaumbele kwa kuisaidia serikali mpya ya Somalia katika vikosi vya ulinzi pia kuimarisha miundombinu wa taifa hilo la pembe ya Afrika.

-DW