Boko Haram Wateka Kambi ya Jeshi Nigeria, Shahidi wa ICC Afariki

Wanajeshi wa Nigeria

Wanajeshi wa Nigeria

MAOFISA nchini Nigeria wamesema kuwa kundi la Boko Haram limeuteka Mji na kambi moja ya kijeshi inayotumiwa na wanajeshi wa kimataifa wanaojaribu kukabiliana na wapiganaji hao. Seneta wa Borno Kazkazini Maina Ma’aji Lawan, eneo la Mji wa Baga amesema kuwa wanajeshi waliitoroka kambi yao baada ya kushambuliwa na Boko Haram jumamosi asubuhi.

Wakaazi wa Baga, ambao walitoroka kupitia maboti hadi taifa jirani la Chad, amesema kuwa raia wengi wameuawa na mji huo kuchomwa. Wapiganaji wa Boko Haram tayari wanadhibiti eneo kubwa karibu na mji wa Baga, ambao hadi kufikia jumamosi ni miongoni mwa miji michache iliokuwa imesalia na serikali.

Wakati huo huo, Maofisa wa polisi nchini Kenya wameupata mwili wa shahidi muhimu wa mahakama ya ICC siku chache tu kabla ya kutoa ushahidi wake katika kesi ya naibu wa rais katika mahakama hiyo. Ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya zinasema kuwa mwili wa Meshash Yebei ulipatikana karibu na mto zaidi ya wiki moja baada ya kuonekana akibebwa na kuingizwa katika gari moja lisilo na nambari za usajili katika Mji wa Eldoret, umbali wa kilomita 200.

Bwana Yebei alitarajiwa kusafiri kuelekea mjini Hague kwa kesi dhidi ya bwana Ruto-Makamu wa Rais ambaye anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mashambulizi dhidi ya watu wa jamii ya kikuyu katika makaazi ya wakalenjin huko Rift valley wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi miaka saba iliopita.
-BBC