SERIKALI ya Nigeria imesema kuwa imefikia makubaliano na kundi la wapiganaji wa Boko Haram kuhusu kuachiwa kwa wasichana waliotekwa nyara wa kutoka Chibok. Mkuu wa Jeshi la Nigeria, Alex Badeh aliyefichua makubaliano hayo mwishoni mwa mkutano wa siku tatu kati ya nchi hiyo na Cameroon ambapo alisema kuwa wanajeshi wa Nigeria watatimiza matakwa ya makubaliano hayo kabla ya kuachiwa kwa mateka hao.
Serikali hiyo imekuwa ikifanya mazungumzo na viongozi wa Boko Haram ili kufikia suluhu. Kwa upande wake Ofisa Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Goodluck Jonathan, Hassan Tukur alisema wajumbe wa serikali walikutana na wapiganaji wa Boko Haram mara mbili nchini Chad chini ya uongozi wa Rais wa Chad Idris Derby.
Alisema kuwa Boko Haram wamekubali kuwaachilia huru wasichana waliotekwa nyara mjini Chibok, hata hivyo, maelezo kuhusu kuachiliwa kwao yatakamilishwa katika mkutano mwingine utakaofanyika wiki ijayo mjini Njamena. Pia alieleza kwamba maafisa wa ujasusi wa Chad walihusika katika mpango huo na kwamba wamethibitisha mazungumzo hayo yamefikiwa na kukubalika na kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau.
-BBC