Bodi ya Wadhamini Muhimbili yatoa masharti makali kwa madaktari

Wauguzi Hospitali ya Muhimbili

*Yawataka madaktari warejee kazini, mwisho Julai 3

BODI ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili imekutana na kutoa maagizo makali kwa uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhusiana na mgomo wa madaktari unaoendelea nchini kote.

Bodi hiyo iliyokutana tanu Juni 28, 2012 imewataka madaktari waliogoma warejee kazini mara moja kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na. 76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, kabla ya uongozi wa hospitali hiyo kutoa adhabu.

Katika taarifa yao kwa uongozi wa Muhimbili, iliyosainiwa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dk. Gabriel Upunda; Bodi imeutaka uongozi kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea na mgomo wakiwemo baadhi yao wanaohudhuria kazini na kutofanya kazi bila sababu za msingi jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kazi.

Bodi hiyo iliyokutana kujadili na kutathmini hali ya utendaji na utoaji wa huduma hivi sasa katika Hospitali ya Muhimbili imewataka madaktari wote waliopo likizo warejee kazini mara moja, huku ikidai tayari utaratibu wa kufidia likizo na nauli umeandaliwa.

“…Uongozi wa Hospitali uwachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi wote watakaoendelea kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi bila sababu za msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za kazi; Uongozi wa Hospitali ufute mara moja ‘rotations’ za Madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo (interns),” ilieleza taarifa hiyo.

Tayari uongozi wa Muhimbili umetoa tangazo kwa madaktari wote kutekeleza maelekezo ya bodi huku ikielekeza madaktari kujiorodhesha kwa wakuu wa vitengo na mwisho wa zoezi hilo ni kesho Julai 3, 2012 saa tatu asubui. Baada ya muda huo kwa madaktari ambao wataendelea na mgomo watachukuliwa hatua za kinidhamu.