BODI YA MIKOPOBYA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU YAONGEZA MUDA WA MAOMBI YA MIKOPO KWA MWAKA WA MASOMO 2013/2014
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawafahamisha waombaji wa mikopo kwa mara ya kwanza, Wanafunzi wanaondelea na masomo na Umma kwa ujumla kuwa muda wa maombi ya mikopo umeongezwa kwa mwezi mmoja hadi Julai 31, 2013.
Pamoja na nyongeza hii ya muda, Bodi inasisitiza waombaji kujaza fomu za maombi ya kwa njia ya mtandao (OLAS) kwa usahihi na kuzingatia muda wa maombi uliowekwa ili kuepuka usumbufu usio wa lazima. Waombaji wa mara ya kwanza wahakikishe wanajaza kwa ufasaha na kuweka viambatanisho vyote muhimu ili kufanikisha mchakato wa uchambuzi na upangaji wa mikopo.
Kundi la kwanza la wanafunzi waliopangwa kulitumikia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao
wamemaliza mafunzo hayo mwezi Juni, 2013 wanapaswa kutumia fursa hii kujaza fomu za maombi ya mikopo bila kukosa. Aidha, kundi la pili la wanafunzi wanaotegemea kuanza hayo mwezi Julai, 2013 walitakiwa wawe wameshaomba mikopo kati ya tarehe 1 Mei, 2013 na 30 Juni, 2013 lakini endapo kuna wachache ambao hawakuweza kufanya hivyo basi nao watumie muda huu wa nyongeza kujaza fomu za maombi kwa njia ya mtandao wakiwa huko huko JKT.
Endapo mwombaji yeyote atakabiliana na matatizo wakati wa kujaza fomu yake anashauriwa kupiga simu kwenye dawati la huduma kwa wateja kwa namba 022 550 7910 kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 2.00 usiku siku za Jumatatu hadi Ijumaa, na kati ya saa 2.00 asubuhi na saa 10.00 jioni siku za Jumamosi.
Ikumbukwe kwamba Bodi haitaongeza muda wa ziada baada ya Julai 31, 2013 ili kutoa nafasi kwa Bodi kuendelea na mchakato wa uchambuzi na upangaji mikopo.
IMETOLEWA NA:
BODI YA WAKURUGENZI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU