Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu Yaongeza Muda wa Maombi

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya mikopo Tanzania, Cosmas Mwaisobwa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bodi ya mikopo Tanzania, Cosmas Mwaisobwa.

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa kupokea maombi ya mara ya kwanza ya mikopo kwa mwezi mmoja zaidi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na HESLB na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, kwa sasa maombi ya mikopo yataendelea kupokelewa kwa mwezi mmoja tena.

“…Nawafahamisha waombaji wa mikopo kwa mara ya kwanza na Umma kwa ujumla kwamba muda wa maombi ya mikopo umeongezwa kwa mwezi mmoja kutoka Julai 1, 2014 hadi Julai 31, 2014,” imesema taarifa ya Bodi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, bodi ilianza rasmi kupokea maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kuanzia Aprili 23, 2014 ambapo tarehe ya mwisho wa kupokea maombi hayo ilikuwa Juni 30, 2014.

“…Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imetoa muda wa nyongeza kwa waombaji wa mikopo kukamilisha maombi ya mikopo katika kipindi cha siku 30, kupitia mtandao kwa anuani: http://olas.heslb.go.tz.”

“…Mwombaji wa mkopo atakayekumbana na matatizo ya kiufundi wakati wa kujaza fomu yake apige simu kwenye dawati la msaada la Bodi kupitia namba 022 550 7910 kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa saa 2.00 asubuhi hadi saa 2.00 usiku, na Jumamosi kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni.”

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa sasa tarehe ya mwisho ya kupokea maombi hayo kwa njia ya mtandao itakuwa ni 31 Julai 2014 na hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza baada ya tarehe iliyoongezwa ku kupita.