Meneja wa Huduma ya Masoko wa Bodi ya Maziwa nchini, Mayasa Simba
Na Joachim Mushi
BODI ya Maziwa Tanzania imesema imeanza kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuhakikisha inaratibu kiwango cha uingiaji wa maziwa nchini ili kulinda maziwa ya ndani.
Kauli hiyo ilitolewa jana katika Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa ndani ya banda la Bodi ya Maziwa na Meneja wa Huduma ya Masoko, Mayasa Simba alipokuwa akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi.
Simba alisema bodi hiyo imeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha bidhaa za maziwa za ndani zinapata soko sawa kiushindani kwa lengo la kukuza kipato cha wajasiriamali wa bidhaa hiyo kutoka ndani na uchumi wa nchi.
Alisema awali TBS ilikuwa ikiangalia ubora tu wa bidhaa hizo zinapoingia ndani huku TFDA usalama wa bidhaa, jambo ambalo liliyanyima masoko maziwa kutoka ndani hivyo na Watanzania kutojenga utamaduni wa kunywa bidhaa za maziwa.
“Tayari tumeanza kusajili kampuni za maziwa kutoka nje, hii itatusaidia kuratibu uingiaji wa maziwa holela na kwa wingi ili kulinda soko la maziwa la ndani, utaratibu huu tumeanza kuutekeleza tangu Mei mwaka huu…lakini changamoto kubwa inayotukabili ni upungufu wa wafanyakazi pamoja na fedha ndani ya bodi,” alisema Simba.
Aidha alisema kwa sasa bodi inatoa mafunzo kwa wajasiriamali nchini ili kusindika bidhaa hizo kwa wingi ili ziendane na ahitaji ya ndani, sambamba na kuongeza uhamasishaji kwa Watanzania juu ya utamaduni wa unywaji wa maziwa na bidhaa zake.
Ofisa huyo masoko aliongeza kuwa kwa sasa Mtanzania mmoja anakunywa lita 43 kwa mwaka za maziwa huku umoja wa mataifa ukishauri kunywa lita 200 kwa mwaka. Hata hivyo ameshauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuanza kuyatumia maziwa kama chakula mashuleni ili kuongeza mahudhurio kwa kuvutia.