Mkurugenzi Mkuu wa Blogu ya Wananchi, William Malecela ‘Le Mutuz’ , akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Blogu ya Wananchi, William Malecela ‘Le Mutuz’ (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu blogu hiyo kutimiza miaka mitatu na semina itakayowakutanisha wasomi wasio na kazi kuhusu namna ya kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Blogu ya Wananchi Media leo inaadhimisha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, sherehe itakayofanyi Hyatt Regency Kempisky zamani Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam Mkurugenzi wa blogu hiyo, Wiliam Malecela (Le Mutuz), alisema kuwa wameamua kufanya sherehe kutokana na mafanikio waliyopata katika kipindi hicho na bendi ya muziki wa kizazi kipya ya THT itatumbuiza.
Alisema licha kufanya sherehe , kutakuwa na semina maalumu ya vijana 300, ambao watakuwa pamoja na matajiri 6 vijana na vijana watatu viongozi wa kitaifa kwa lengo la kubadilishana mawazo na matajiri na viongozi hao, ambao wataeleza walivyopigana mpaka kufikia walipo kimaisha.
Alisema alianzisha blogu hiyo baada ya kuisajili kwa msajili wa makampuni (Brela) 2012, ikianza kwa kutembelewa na watu 200 kwa siku lakini kwa sasa inatembelewa na watu 70,000 mpaka 100,000 kwa siku kitu ambacho anajivunia na kuwashukuru wadau.
Kampuni hiyo ilianza kwa mtaji wa dola ya Marekani 500, ikiwa na usajili wa makampuni wa Brela, na inatoa ajira kwa vijana 4 waliomaliza vyuo vikuu nchini na ina ofisi yake katika jengo la Tancot House Sokoine Drive, Dar es Salaam.
Alisema katika miaka mitatu blogu imeweza kuwa na domain yake yenyewe ya www.williammalecela.com na kuingia kwenyeFacebook, Twitter, na Instagram ambapo sasa inarusha habari sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja na kuweza kuwafikia watu hadi 500,000 kwa siku.
Alisema mipango ya baadaye ni kuwekeza kwenye kampuni mpya ya African Swahili Media Radio & Television ambayo tayari imeshapata leseni ya kufungua radio na televisheni ambayo inatazamiwa kuwa hewani Aprili mwaka huu, huku kituo cha radio kitakuwa Morogoro na televisheni jijini Dar es Salaam.