Bloggers Tanzania ‘Wampigia’ Magoti Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza.

Na Mwandishi Wetu

MTANDAO wa waandishi wa habari za mitandao Tanzania (Bloggers Network-TBN) umemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete kutumia mamlaka yake kutoupitisha muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni. 
 
Kwa mujibu wa taarifa ya TBN iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari imesema Muswada wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaotaka kupitishwa unakandamiza uhuru wa habari ikiwa ni pamoja na kulipa nguvu kubwa Jeshi la Polisi zaidi ya mahakama.

Katika sheria hiyo, Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi anauwezo wa kupekuwa na kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao jambo ambalo linaweza kutumiwa na taasisi hiyo vibana na kuwakandamiza wanahabari. TBN inahoji kwanini polisi apewe mamlaka ya kumsulubisha mtuhumiwa katika hatua ya mwanzo bila uthibitisho sahihi juu ya kosa lake?
 
“…TBN imeshtushwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati ya dharura kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu kipya nchini hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia na Serikali ili wengi watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na yapi yanakubalika.”
 
“Kimsingi TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na wanamitandao ya jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria isiyo na viashiria kandamizi juu ya uhuru wa kupata na pokea habari,” inaeleza taarifa hiyo ya TBN kwa vyombo vya habari.
 
Hali kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu zenye uzito za kwanini sheria hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa dharura bila ya kupata majibu.
 
“Mbali na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia maadili ya kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni kutunza siri ya chanzo cha habari yake hadi pale inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari. Kupitia sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini kutokana na kwamba sheria inaainisha ni kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.”
 
Aidha, TBN imemuomba Rais Kikwete pia kusitisha Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013 ambao pia unaingilia uhuru wa taarifa kwa wanahabari, kwani unavinyima uhuru vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu mbalimbali.

“…Kama ilivyo Ibara ya 7(4), ‘Chombo chochote cha habari ambacho kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au kinatangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa.’’
 
Hali hii inamaanisha hata blog zote ziko hatarini kuelekea katika kulazimika kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza takwimu zilizopitiwa na serikali tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa habari nchini.