Bingwa wa Vodacom Cycle Challenge 2011 Tanga apatikana

Naibu Meya wa Mkoa wa Tanga Seleboss Mustafa akimkabidhi fedha taslimu sh. 150,000 mshindi wa kwanza wa mbio za Vodacom Tanga Cycle Challenge wa kilomita 140, Hassan Sharif (kulia) mara baada ya kuibuka kidedea katika mbio hizo kwa kutumia muda wa masaa 4:13.07 wapili toka kushoto Ofisa Udhamini wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude na Msimamizi wa Mawakala Kanda ya Kaskazini, Michael Kasun.

HASSAN Shariff amefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya mbio za baiskeli ya “Vodacom Tanga Cycle Challenge 2011” baada ya kumaliza mwendo wa umbali wa kilomita 140 akiwa mbele ya washiriki wengine.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya Wakati Sports Promoter
na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania yalishirikisha makundi matatu ambayo ni ya baiskeli zilizotengenezwa maalumu kwa michuano ambapo washiriki walipita Wilaya za Muheza na Korogwe na kurejea Tanga mjini umbali wa kilomita 140.

Sharrif alitwaa ubingwa huo akiwa katika kundi la baiskeli maalumu za
mbio hizo ambapo alimaliza michuano hiyo akiwa amekimbia kwa saa 4.13.07 na kufuatiwa na Juma Kashinde aliyetumia muda wa saa 4.14.52 wakati mshindi wa tatu alikuwa Revecatus Sebastian aliyemaliza akiwa amekimbia kwa saa 4.15.30.

Naibu Meya wa Mkoa wa Tanga, Seleboss Mustafa akimkabidhi fedha taslimu sh. 100,000 mshindi wa kwanza wa mbio za Vodacom Tanga Cycle Challenge wa kilomita 80, Kadushi Nkandi (kulia) mara baada ya kuibuka kidedea katika mbio hizo wapili toka kushoto Ofisa Udhamini wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude na Msimamizi wa Mawakala Kanda ya Kaskazini, Michael Kasun.


Nafasi ya nne ilikwenda kwa Hamis Milikioni aliyekimbia kwa saa
4.28.08, Mathew Alberto alimaliza akiwa amekimbia kwa saa 4.35.06 huku Athumani Muya akikimbia kwa saa 4.38.07.

Kundi la baiskeli za kawaida lilianzia Tanga mjini kupitia Tanganyika Wilaya ya Muheza umbali wa kilomita 80 ambapo Kadushi Nkandi aliongoza kwa kutumia muda wa saa 1.56.00, Issa Kashinde alishika nafasi ya pili kwa kumaliza akiwa ametumia muda wa saa 1.57.12 huku Mohamed Bundala alitumia saa 2.15.13.

Baiskeli za miguu mitatu zilikuwa za kulizunguka jiji la Tanga
ambapo aliyeongoza ni Jackson Kinyusa aliyekimbia kwa dakika 30.20
akifuatiwa na Mohamed Balozi dakika 32.16 huku Medrin Sabuni akishika
ushindi wa tatu kwa kukimbia kwa dakika 45.02.

Mgeni rasmi ,Mohamed Mustapher ambaye pia ni diwani wa Kata ya
Nguvumali na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Wilaya ya
Tanga,aliipongeza kampuni ya Vodacom kwa kuukumbuka mchezo wa baiskeli na kuwaomba kuboresha zaidi mwakani kwani Tanga ni mkoa wenye vipaji vingi.

Mgeni huyo ambaye alimwakilisha Meya wa Jiji la Tanga alimkabidhi
Shariff kiasi cha sh 150,000, Kashinde sh 100,000, Revocatus sh 75,000
wakati washindi wa kwanza katika makundi ya baiskeli za miguu mitatu
na za kawaida walizawadiwa sh 100.000, wa pili sh. 75,000 wa tatu sh
50,000 huku washiriki wengine wakipewa kifuta jasho cha sh. 10,000 kwa kila mmoja.

Ofisa Udhamini wa Vodacom, Ibrahim Kaunde alisema huu ni mwaka wa pili kwa Kampuni yake kudhamini mashindano ya baiskeli kwa Mkoa wa Tanga na Mwanza lengo likiwa ni kuimarisha mchezo huo katika maeneo hayo kwa kuwa unaonekana kupendwa zaidi.

“Kimsingi Vodacom imejikita kudhamini michuano ya baiskeli Tanga na
Mwanza kutokana na ari na mwamko uliopo kama ambavyo tunavyodhamini riadha mkoani Kilimanjaro”alisema Kaunde.