Na Mwandishi Wetu,
BIFU la wanamuziki nyota wa muziki wa bongo fleva kati ya msanii Nasibu Abdul a.k.a Diamond Platnumz na msanii Ali Kiba limeendelea kushika kasi na sasa limeingia kwa mashabiki na wapenzi wa wasanii hao. Bifu hilo lilipamba moto zaidi katika tamasha la fiesta jijini Dar es Salaam ambapo msanii Diamond alizomewa mwanzo mwisho na baadhi ya mashabiki katika tamasha hilo huku baadhi ya watu wakidai waliofanya kitendo hicho ni mashabiki wa msanii Ali Kiba na walidhamiria kitendo hicho.
Diamond akiwa katika mavazi ya kijeshi ambayo hadi sasa yamemletea soo na kesi ambayo bado anakabiliana nayo pamoja na vijana wake, alijikuta akizomewa katika tamasha la fiesta na baadhi ya mashabiki kitendo ambacho yeye amekichukulia ni kama changamoto katika fani hiyo na tayari amekipuuza.
Mashabiki waliomzomea mwanamuziki huyo walisikika akipaza za kuzomea huku wakiimba; ‘Kiba, Kiba, Kiba Kiba’ wakitaka nyota Diamond Platnumz ashuke jukwaani na kupanda Ali Kiba ambaye alitumuiza naye katika tamasha hilo. Hata hivyo zomea zomea hiyo ilizidi kuchochea hasira za wapenzi na mashabiki wa Diamond ambao kesho yake walianza kutupiana maneno kupitia mitandao ya kijamii huku kila mashabiki wakifagilia na kuvutia upande wao.
Kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii mashabiki wa Ali Kiba waliandika kuwa Diamond hata avume vipi hawezi kufikia nyota ya Kiba wala uwezo alionao staa huyo wa muziki wa kizazi kipya. Waliandika nyodo anazozitoa Diamond kwa Kiba ni kazi bure hivyo kumshauri aache tabia hiyo na badala yake afanye muziki. Wale wa Diamond waliandika kuwa Kiba alichezea nafasi yake kipindi akivuma kimuziki hivyo kwa sasa hawezi kufikia anga za msanii Diamond huku wakimtaka awe mpole na kuacha kuendeleza bifu hilo.
“…Diamond yupo juu kuliko Ali Kiba kama unabisha chukua hii, Mlimani City kapiga show kiingilio 50,000, Dodoma kapiga show kingilio 30,000 na hamkuona show ya BBA jamani ila wabongo wivu tu na kuhusu mavazi yanayofanana na jeshi (JWTZ) suala hili mashabiki haliwahusu anajua yy kwanini kavaa na kwa idhin ya nani…” aliandika shabiki mmoja wa Diamond.
“…Mashabiki wanapo zomea ni njia mojawapo ya kuonesha kuna kitu fulani ambacho hakipo sawa. Au kimekuwa ni kinyume na matarajio yao. Ndiyo maana wasanii wakomavu huwa wanatoa ‘press release’ ktk matukio kama haya. Especially kuomba msamaha mashabiki wao. Kwa kuwa wanajua watakuwa wameumia nafsi zao. Na wakati mwingine tukio linaloongelewa halihusiani kabisa na fani ya msanii,” aliandika shabiki mmoja.
Shabiki mwingine aliandika; “…Kutokana na watu kutokuwa na hoja za msingi ndio maana wengine tunashawishika kuamini kwamba wengi wao wanasukumwa na chuki na wivu kwavile mtu asiye na husuda hawezi kuombea kuona mtu mwingine anaanguka tena kwa sababu ambazo wala hazikuhusu moja kwa moja!
“Tatizo kubwa hapa bongo, msanii yeyote akikataa kuburuzwa….ndio wanaanza kumfanyia fitina za kumshusha kisanii, tuliona kwa Sugu, Jaydee na sasa Diamond, hawa ni wasanii wanaojielewa, na wanajua nini wanafanya, mbona Mwz hakuzomewa na sehem zingine pia hakuzomewa, hapo ndio ufahamu ya kuwa wazomeaji wote walilipwa posho…..,” aliandika shabiki mmoja kwenye mtandao wa jamii.