Na Aron Msigwa –MAELEZO
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecki Sadiki amewaagiza viongozi na watendaji wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanaovunja sheria za jiji kwa kuendesha shughuli mbalimbali za biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa. Sadiki amewataka waendesha pikipiki ‘Bodaboda’, Bajaji, waendesha baiskeli na mikokoteni wanaofanya biashara ya kubeba abiria na mizigo maeneo yasiyoruhusiwa kisheria ikiwamo katikati ya jiji kuondoka wenyewe kabla hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Jiji la Dar es Salaam limeamua kuchuakua uamuzi huo kufuatia tatizo la baadhi ya wananchi kuamua kuvunja sheria zilizowekwa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na kutafuta fedha hali inayoleta usumbufu na kero kwa wananchi wengine.
Alisema licha ya changamoto inayolikabili Jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya katikati ya Mji hali iliyopo sasa ya biashara holela na uvunjifu wa sheria unaofanywa na waendesha Bodaboda, Bajaji, baiskeli, mikokoteni na Taxi bubu maeneo yasiyoruhusiwa kisheria hauwezi kuvumilika.
“Jiji la Dar es Salaam tumekuwa na kero ya muda mrefu hasa ya ombaomba, waendesha baiskeli, bodaboda na wafanyabiashara katika maeneo ya makutano ya barabara yasiyoruhusiwa hali hii hatuwezi kuivulimia, sisi hatufukuzi watu bali tunawataka wafuate sheria za Jiji,” alisisitiza.
Aidha alisema Serikali haina lengo la kuwazuia wananchi kufanya biashara na shughuli nyingine za kujiingizia vipato kama wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuongeza kuwa wale wote wanaoomba leseni za kufanyia biashara wanapewa taratibu na miongozo na masharti ya kuzingatia wanapofanya biashara zao jambo ambalo wengi wao wanashindwa kulizingatia.
“Kila Manispaa ina miongozo na kanuni za uendeshaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kutenga maeneo ya biashara na kuwaruhusu wale wanaokidhi masharti ya leseni zao kufanya biashara zao ila wengi wao hasa madereva wa Bajaji na Bodaboda hawazingatii haya,” Alisema Sadiki.
Aliongeza kuwa sheria zote zilizotungwa zimewekwa ili zifuatwe kwa ustawi wa taifa na si vinginevyo na kubainisha wote waliovamia maeneo ya vituo vya mabasi, maeneo ya vituo vya umeme na hifadhi za barabara ni vema wakaondoka wenyewe na kukubali kutii sheria bila shuruti huku akitoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara na wauza vyakula ‘mama lishe’ walio anza kuvamia maeneo ya ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo Kasi (DART).
“…Haiwezekani sheria za jiji zikavunjwa na sisi tukaendelea kuwaangalia baadhi yao wamefikia hatua ya kuvamia maeneo ya mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuanza kufanya biashara na kuwasumbua mafundi jambo lisilokubalika,” alisema.
Akizungumza kuhusu biashara ya bodaboda inayofanywa na vijana wengi jijini Dar es Salaam, Sadiki ameeleza kuwa mpango wa Serikali kuruhusu bodaboda na bajaji kutumika kubeba abiria ulikuwa na lengo zuri la kuwawezesha wananchi kupata usafiri hasa katika maeneo yasiyofikika kirahisi kwa magari kama vijijini na kuongeza kuwa itakua na mafanikio kama wahusika watafuata sheria.
“Serikali iliruhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji kutumika kubebea abiria kwa nia nzuri ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafiri na kuongeza ajira, hivyo siyo nia yetu kuwadhalilisha vijana hawa tunachowataka wafanye ni kufuata sheria za nchi,” alisema.
Aidha kwa upande wa ongezeko la ombaomba ambao baadhi yao walirudishwa katika maeneo yao ya awali na kurejea tena jijini Dar es salaam ameeleza kuwa utaratibu wa kuwafuatilia uko pale pale na kufafanua kuwa watakaokutwa na makosa ya kukaa maeneo yasiyoruhusiwa watafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna (CP) Suleiman Kova alisema ni wakati sasa wa wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria na kusisitiza kuwa ni vema wananchi wakajenga mazoea ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo vya kuwawezesha kutembea barabarani.
“Kwa waendesha pikipiki “bodaboda” hali ni mbaya wengi wameumia na kupata ulemavu wa kudumu kwa kutozingatia sheria za usalama barabarani na kukidhi matakwa ya kuendesha pikipiki hizo,”
Alisema Jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa kushirikiana na manispaa zote tatu kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa sheria vinakomeshwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona dalili zozote za uvunjifu wa amani hasa matukio ya ujambazi kwa kutumia pikipiki yayoendelea kuongezeka kwa kasi.
“Napenda niwahakikishie wananchi kuwa jeshi la polisi tumejipanga vizuri kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu wa aina zote, pia natoa wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam hasa wafanyabiashara kuepuka kutembea na fedha nyingi ili kuepuka madhara ya kuvamiwa,” alisema Kova.
Naye Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki, Conrad Shio alisema sheria ya usafirishaji kusimamia Bajaji na Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wake na pia waendesha pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa kuzingatia kanuni taratibu na kanuni zilizowekwa. “Sisi kama SUMATRA tunaendelea kufanya kila tuwezalo kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjivu wa sheria za barabarani,” alieleza.