HATIMAYE mwana mama Theresa Mary May amechukua usukani na kuwa Waziri Mkuu wa taifa la Uingereza.
Akizungumza baada ya kupokea ufunguo wa makao rasmi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi. May amewahakikishia washirika wake na mataifa ya muungano wa ulaya kuwa licha ya taifa hilo kuamua kujiondoa, Uingereza imedhamiria kuungana na mataifa washirika na kutekeleza wajibu wake katika muungano wa mataifa huru duniani.
Alisema kuwa serikali yake haitakubali kuegemea upande mmoja kwa kuwasikiliza matajiri pekee na kuwasahau wananchi wa kawaida. May alisema kuwa serikali atakayoiunda itahakikisha inatimiza matarajio ya kila raia wa Uingereza ili kujenga usawa.
Aliwakumbusha wakosoaji wake maana ya jina rasmi ya chama chake ambacho ni Chama cha Conservative. Waziri huyo mkuu ameapa kuangamiza udhalimu wa aina yeyote ima ni kwa misingi ya ubaguzi wa rangi jinsia ama kiwango cha mapato.
Bi Theresa May anakuwa Waziri Mkuu wa 13 kuwahi kuiongoza taifa la Uingereza katika enzi ya Malkia Elizabeth wa pili. Malkia tayari amempa idhini ya kuunda serikali mpya muda mchache tu baada ya kujiuzulu rasmi kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. David Cameron.
Yeye ndiye mwanamke wa kwanza kuhudumu kama Waziri Mkuu tangu mtangulizi wake Margaret Thatcher atoke madarakani.
-BBC