Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT) limeandaa mashindano ya ngumi ya Klabu Bingwa ya Taifa yanayotarajia kufanyika kuanzaia Novemba 26 hadi 30, 2012. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BFT, inasema mashindano hayo yatahusisha vilabu vya ngumi vilivyosajiriwa na kutambuliwa na BFT kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na taasisi za vyombo vya ulinzi na usalama kwa mujibu wa katiba yake.
“Timu zote zitakazoshiriki zitatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa barua na kutuma picha za mabondia na viongozi kabla ya Novemba 11, 2012 kwenye ofisi za BFT zilizopo Dar es Salaam kwa mipango zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha BFT imesema itaandaa kozi kwa ajili ya waamuzi wa ngumi wa mashindano hayo, itakayofanyika jijini Dar es salaam. Taarifa hiyo imefafanua zaidi kuwa makocha watakaotumika ni wale waliohudhuria kozi na wanatambuliwa na BFT, na kila timu itaruhusiwa kuwa na timu meneja 1, daktari 1 na physiotherapist 1.
Imesema raundi kwa kila mchezo ni tatu, na kila roundi itakuwa ikichezwa kwa dakika tatu, huku muda wa mapumziko ukichukua dakika moja kwa wanaume; na kwa wanawake ni kwa mjibu wa sheria za AIBA.
“…Kila timu itatakiwa kuja na waamuzi wawili waliohudhuria kozi na wanatambuliwa na BFT. Chama cha waamuzi Tanzania kitateuwa waamuzi wengine wa Taifa watano kuja kuungana na waamuzi watakaokuja na timu.
“Kila mchezaji atatakiwa kuwa na Record book yake atatakiwa kuwa nayo wakati wa zoezi la kupima uzito na afya. ‘Accreditation card’ ambazo zitatumwa kwa timu na BFT baada kutuma majina na picha za washiriki wote.”
Aidha taarifa ilisema kila bondia atatakiwa kuwa na jozi mbili za kuchezea bluu na nyekundu, bandeji za mikononi, mouth guard, soksi na viatu vya ulingoni. BFT itatayarisha Gloves za kuchezea, heard gurds, cup protector, ulingo wa kuchezea, ukumbi wa kuchezea na huduma za matibabu.
Hata hivyo ada ya ushiriki wa mashindano kwa kila timu ni sh. 200,000 na kila timu itatakiwa kujigharamia usafiri, chakula na malazi wakati wote wa mashindano.
“…Katika mashindano hayo tutachagua wachezaji watakaofanya vizuri kuwaongeza katika kikosi cha timu ya taifa kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya ubingwa wa dunia ,jumuiya ya madola,mashindano ya Afrika na Olimpiki.