SHIRIKISHO la ngumi Tanzania (BFT) halitambui uongozi uliojiingiza madarakani wa kuongoza chama cha ngumi mkoa wa Dar es salaam ( DABA ) kiujanja ujanja bila kuzingatia Sheria na Kanuni za Baraza la Michezo Tanzania (BMT) , katiba ya Chama cha ngumi cha dunia (AIBA), Shirikisho la ngumi Tanzania (BFT) na katiba ya Chama cha Ngumi mkoa wa Dar es salaam (DABA).
Uongozi huo ulijingiza madarakani tarehe 21/09/2013 katika ukumbi wa DDC Mlimani bila ya kuwa na kibali cha kutoka BFT wala Kibali kutoka Ofisi ya afisa michezo wa mkoa wa Dar es salaam, ambao wao kiutaratibu ndio walikuwa na mamlaka ya kutoa kibali cha Kufanyika kwa uchaguzi huo na kuusimamia kwa mujibiu wa sheria zinazoongoza michezo hapa Tanzania.
Badala yake genge la watu wachache walijikusanya na kupeana fomu kinyume na taratibu kwa kujuana na hatimaye kupeana taarifa wakakutana na kujivika madaraka kwa nyadhifa mbalimbali bila kufata taratibu.
BFT haikubaliani na jambo hilo kwa kuwa kati ya waratibu wa zoezi hilo waliojivika uongozi wa juu ni wale waliokuwa katika uongozi wa shirikisho la ngumi Tanzania BFT na kupelekea Tanzania kufungiwa uanachama na chama cha ngumi cha dunia (AIBA) kwa miaka miwili na zaidi kusababisha bondia aliyekuwa tegemeo na Taifa Petro Mtagwa kufungwa jela miaka 15 nchini Mauritius pia kusababisha bondia Emillian Patrick kushindwa kushiriki Mashindano ya Olimpiki 2008 baada ya kuwa amefuzu kwa tuhuma za kula njama za kusafirisha madawa ya kulevya.
Kibaya zaidi wengi waliopewa madaraka hawakuja fomu za kuomba nafasi kama walivyopewa na hawakuwepo katika uchaguzi huo, wala hawakufanya usaili kama taratibu zilivyo.
Wanachama halali waliokuwa wanatakiwa kuwepo katika uchaguzi huo mfano viongozi wa chama cha ngumi Temeke hawakupewa taarifa za uchaguzi na wameleta malalamiko ofisi za BFT.
Uchaguzi huo umekiuka katiba kwa kuhusisha mabondia na viongozi wa ngumi za kulipwa kitu ambacho ni tofauti na katiba zote za ngumi za ridhaa.
BFT itachukua hatua kali za kimaadili na kinidhamu kwa wote waliohusika na zoezi hilo na kusisitiza kwa wanachama wote kuzingatia sheria za uchaguzi wanapofanya uchaguzi wa vyama vyao na kuwataka wengine kutokujiingiza kwa magenge ambayo historia inaonyesha wamekuwa wasubufu wa mambo mbalimbali tokea uongozi wa Narcis Tarimo enzi za TABA kwa masilahi yao binafsi.
Zaidi tutashirikiana na Ofisi ya Afisa michezo wa Mkoa kuhakikisha uchaguzi unafanyika wa kupata viongozi kwa kuzingatia taratibu.