BENKI ya Posta Tanzania (TPB) imetoa mchango wa madawati na viti 50 vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni Nane kwa Shule ya Sekondari ya Ikoma, iliyopo Wilayani Serengeti Mkoani Mara. Mchango huo wa madawati ulikabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu na Afisa Mtendaji Mkuu wa (TPB) Sabasaba Moshingi, kwenye hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Sabasaba Moshingi alisema kuwa benki yake imeamua kutoa viti pamoja na madawati hayo ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaoanza kutumia shule hiyo hapo mwakani watakaa kwenye mazingira mazuri yanayofaa.
Pia alitoa pongezi nyingi kwa uongozi wa Kijiji hicho cha Ikoma kwa bidii zao zilizohakikisha kuwa wanakamilisha ujenzi wa madarasa pamoja na maabara, tayari kwa kupokea wanafunzi mwaka ujao. Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi huo ili kuweza kukabiliana na changamoto nyingine kama vile uhaba wa nyumba za waalimu na mabweni zinazoendelea kuikabili shule hiyo.
Naye mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo Mhe. Nurdin Babu aliishukuru Benki ya Posta kwa msaada huo uliofika wakati muafaka, ambapo shule hiyo inajiandaa kupokea wanafunzi wapya. Alisema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania mwenye mapenzi mema kuhakikisha kuwa anatoa kipaumbele kwa sekta ya elimu ili kuwawezesha watoto wetu kupata elimu kwenye mazingira mazuri. Alitoa wito kwa taasisi nyingine kuendelea kuchangia sekta ya elimu hususan shule hiyo, ili waweze kutatua changamoto nyingi zinazoikabili shule hiyo.