BENKI ya Posta Tanzania (TPB), Tawi la Tunduma imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Tunduma, wilayani Momba. Semina hiyo iliyohudhuriwa na wajasiriamali wapatao 100, ililenga kuwaelimisha wafanyabiashara hao kuhusu matumiza mazuri ya huduma za kibenki, hususan mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Momba Abiudy Saideya, aliipongeza Benki ya Posta kwa kutoa mafunzo ambayo alisema yanawasaidia wafanyabiashara wa Tunduma kukuza uelewa wa matumizi sahihi ya huduma zinazotolewa na taasisi za fedha.
Aliwashauri wafanyabiashara wachukue mikopo ili kukuza mitaji yao na kuongeza uzalishaji, lakini bila kuwa na elimu sahihi juu ya matumizi ya mikopo hiyo faida yake inaweza isipatikane. “Nawashauri wafanyabiashara mnaohudhuria semina hii kutimia fursa hii kujadiliana na benki ya Posta ili mfikie muafaka katika huduma mnazozitaka,” alisema Mkuu wa Wilaya hiyo.
Aidha aliwaasa wafanyabiashara kujiepusha na biashara haramu zitokanazo na bidhaa haramu zilizozagaa mpakani mwa wilaya yao, kwani kufanya hivyo bishara zao zinaweza kutaifishwa na hivyo kupoteza mitaji yao bila kujua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya Posta, Henry Bwogi iliwasisitiza wafanyabiashara hao kutembelea tawi la benki hiyo lililopo Tunduma ili kujipatia huduma zote za kibenki hususan mikopo itakayowawezesha kukuza mitaji yao. Pamoja na hayo aliongeza kuwa benki ya TPB inatoa mikopo ya aina nyingi, kuanzia ile ya vikundi hadi ya wafanyabiashara wakubwa, huku riba zinazotozwa na benki hiyo ni nafuu sana.