WAZIRI wa Kazi na Ajira nchini Tanzania, Gaudensia Kabaka ameipongeza Benki ya Posta Tanzania (TPB) pamoja na Mfuko wa PSPF kwa kushirikiana na kuanzisha mpango wa utoaji wa mikopo ya elimu kwa vijana pamoja na mkopo wa kuanzia maisha kwa wafanyakazi. Waziri Kabaka ametoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizinduwa huduma ya mkopo wa elimu kwa wanachama wa mfuko wa PSPF iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Jubelee Tower.
Alisema huduma za mikopo ya elimu na kuanzia maisha ni huduma muhimu sana kwa vijana kwani upataji wa fedha za kujiendeleza kwa kundi hili imekuwa changamoto kubwa hivyo kupatikana kwake itafungua milango kwa vijana kujiendeleza kielimu bila vikwazo.
Akizungumzia huduma ya mkopo wa wa kuanzia maisha alisema huduma hiyo imekuja wakati muafaka kwani mtu anapoanza kazi anakuwa akihitaji vitu muhimu na vya msingi katika maisha lakini wamekuwa wakikwamishwa na hali ya kipato. Hivyo mkopo huu utakuwa mkombozi wa wengi wanaoanza maisha kazini.
“…Kitu kilichonifurahisha zaidi ni jinsi PSPF mlivyoshirikiana na Benki ya Posta Tanzania katika kubuni, kupanga, kuandaa na hatimaye kutekeleza utaratibu huu, hili ni jambo sahihi na muafaka kwani kwa mujibu wa taratibu za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii duniani kote kazi za mifuko hii sio kutoa mikopo bali ni kuwawezesha wanachama wake kupata mafao yao stahili pale wanapostaafu,” alisema Waziri Kabaka.
Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa kushirikiana na Mfuko wa PSPF imezinduwa aina mpya ya mikopo kwa wanachama wake ambapo watapata fursa ya kupewa mikopo ya elimu pamoja na ya kuanzia maisha kwa wale wafanyakazi wanaoanza maisha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania, Sabasaba Moshingi alisema TPB inatambua mzigo mkubwa uliobebwa na Serikali katika kuwasomesha vijana hivyo imeamua kubeba jukumu la kuwasaidia vijana kukopa kwa lengo la kujiendelea kielimu.
“Benki ya Posta inatambua mzigo mkubwa uliobebwa na Serikali katika kuwasomesha vijana wetu katika vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini, na tukiwa kama Benki halisi ya Kitanzania tumeamua kwa dhati kabisa kuisaidia Serikali katika nyanja hii, tukishirikiana na wenzetu wa PSPF,” alisema Moshingi.
Alisema hata hivyo Benki ya Posta imeendelea kubuni huduma za kibenki mbalimbali kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi wa kila kada hapa nchini. Alisema Mwezi Machi 2014 benki hiyo iliingiza huduma mpya ya mikopo kwa kundi la wastaafu nchini jambo ambalo limekuwa faraja kubwa kwa wastaafu nchini.
“…Adhma yetu ni kuhakikisha kuwa tunamkomboa kiuchumi mwananchi, hususan mwenye kipato cha chini kwa kumpatia mkopo wenye riba nafuu. Mkopo huu wa elimu uliozinduliwa leo una lengo la kumsaidia mwanachama wa PSPF kutimiza ndoto zake kwa kujiendeleza kielimu katika ngazi yoyote, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na nyinginezo,” alisema.
“Mwanachama wa PSPF anayetaka kukopa aina hii ya mkopo atadhaminiwa na mwajiri wake, pia mkopo huu unabima, hivyo endapo mkopaji atafariki familia yake haitaendelea kudaiwa na riba inayotozwa kwa mkopo huu ni nafuu yaani asilimia 14 tu kwa mwaka,” alisisitiza Moshingi.