Benki ya Exim China Yaipa Mkopo Tanzania Trilioni 16

1

Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati hapa nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Julai, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.

Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.

“Kuhusu huu mradi wa reli ya kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda”Amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.

Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Congo.

“Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika kimataifa, na wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.

“Na kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari zetu” Amesema Rais Magufuli.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda-Kalemela, Tabora-Uvinza-Kigoma na Isaka-Keza-Msongati.

Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
20 Julai, 2016

2

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha pamoja na ujumbe wa Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

3

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akimshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

4

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang kutoka kulia mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma. Wengine katika picha ni wakwanza kushoto ni Balozi wa China hapa nchini Lu Youqing, Waziri wa Fedha na Mipango Filipo Mpango, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Suzan Kolimba.

5

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang watatu kutoka kulia mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma

6

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

7

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiagana kwa furaha na Rais wa Benki ya Exim ya China Liu Liang katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

Picha na Ikulu