RAIS wa Benki ya Exim ya Nchini China Bw. Liu Liang amesema Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufadhili miradi ya maendeleo ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya China na Tanzania unaolenga kuboresha, kujenga na kuinua uchumi imara kwa wananchi wa Nchi hizo.
Bw. Liang amesema hayo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa Jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua kituo mahiri cha Kuhifadhia Kumbukumbu (Internet Data Centre), kilichopo eneo la Kijitonyama ambacho ujenzi wake umefadhiliwa na benki hiyo.
Aidha amesifia kazi nzuri inayofanywa na Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ambayo itawaletea wananchi wake maendeleo ya haraka kwa kipindi kifupi.
“Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya kwa kusimamia vizuri fedha zinazotolewa na wahisani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na hivyo kutushawishi sisi kama benki ya Exim kuendelea kutoa fedha kwa miradi mbalimbali ya maendeleo”, amesema Bw. Liang.
Kwa upande wake Waziri Profesa Makame Mbarawa (Mb) ameipongeza Serikali ya China kupitia Benki hiyo kwa kuwa wadau wakubwa wanaochangia fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kuomba ushirikiano huo uwe endelevu kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayesimamia sekta ya Mawasiliano) Prof. Faustine Kamuzora amesema maendeleo makubwa kwenye ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamesababisha uzalishwaji mwingi wa data hivyo Serikali na Sekta mbalimbali wanahimizwa kutumia kituo hicho mahiri cha kuhifadhia kumbukumbu zao kwani zitakuwa salama.
Amesema huduma ya mtandao katika kituo hicho imeimarishwa kutokana na kuunganishwa na mkongo wa taifa na hivyo itawarahisishia wateja wake kuweka na kuchukua taarifa kwa haraka. Kituo cha kutunza Kumbukumbu (Internet Data Centre) ambacho ni cha kwanza kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni fursa mpya kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi kuzihifadhi na kuzitumia wanapozihitaji, kinalimikiwa na Serikali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano