WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amewafukuza kazi mawaziri wawili ambao ni waandamizi na viongozi wa vyama katika serikali yake ya mseto jambo ambalo linatafsiriwa kuwa ameiweka nchi katika hali ya kufanyika mapema uchaguzi wa bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari kupitia televisheni, Netayahu amewashutumu mawaziri hao wawili akiwemo Waziri wa Fedha, Yair Lapid, na Waziri wa Sheria, Tzipi Livni kuwa walipanga njama ovu dhidi yake.
Netanyahu alisema kuwa amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia madhara yanayoweza kusababishwa na kitendo wanachokifanya viongozi hao. “Katika neno moja yanaitwa maasi, na hayo yanafanya isiwezekane kuendesha serikali, iwe vigumu kuongoza nchi, kwa hiyo muda mfupi uliopita nilimwagiza Katibu wa Baraza la Mawaziri kutoa barua za kuwafukuza kazi mawaziri Livni na Lapid. Pia kutokana na ulazima wa kuhakikisha kunakuwepo serikali imara na yenye kufuata maadili, nimeamua kusukuma mbele sheria ya kuvunja bunge na kwenda katika uchaguzi haraka iwezekanavyo.” alisema Waziri Mkuu Netanyahu.
Wanasiasa wote wawili viongozi wa vyama vya mrengo wa kati, wamesema nchi imetumbukizwa katika uchaguzi usio wa lazima. Taarifa zinadokeza huenda Netanyahu akataka utawala mpya utakaovihusisha vyama vya dini vinavyowakilisha madhehebu ya Wayahudi wa ultra-orthodox.
-BBC