Basi la Ngorika laua tisa na kujeruhi 16

Na Mwandishi Wetu
Arusha

WATU 9 wamefariki dunia na wengine nane kujeruhiwa huku wanne kati
yao wakiwa na hali mbaya, baada ya magari waliyokuwa wakisafiria
kugongana na kupinduka katika eneo la Makumira wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye,
alisema kuwa tukio hilo limetokea leo majira ya saa 12:30 asubuhi nje kidogo ya Mji wa Arusha.

Alisema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota hiece lenye namba za usajili T 773 BGT lililokuwa likiendeshwa na Selemani Juma (30) mkazi wa Kijenge na basi la Ngorika aina ya Scania namba T 633 ANF lililokuwa likitokea Arusha kwenda Dar es Salaam, likiendeshwa na Emanuel Mchoro (30) mkazi wa Mwanga, Kilimanjaro.

Kamanda Andengenye alisema alisema ajali hiyo ilitokea baada ya haice
kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake akiwemo mwendesha baiskeli, hata hivyo kabla hajalipita aliona basi la Ngorika likija kwa kasi ndipo alipoamua kuingia porini ili kujinusuru asigongane uso kwa uso na gari hilo.

Hata hivyo kabla dereva wa haice hajafika mbali akiiacha barabara basi la Ngorika lilimgonga ubavuni na kusababisha watu 9 waliokuwa ndani ya gari hilo kufariki dunia papo hapo akiwemo dereva wa basi la Ngorika.

Andengenye aliwataja marehemu hao kuwa ni, Kizo Rafael Ndosi (35)
mkazi wa Arumeru, Patriki Temba (28), Samsoni Emanuel Minja (60), Hamisi Charles (30), Huruma Safiel (28) wote wakazi wa Usariver na John Kess (38) mkazi wa Majichai.

Wengine ni Emanuel Mchoro (30) mkazi wa Mwanga ambaye ni dereva
wa Ngorika na Fatuma Msuya (35) mkazi wa Usariver ambaye ni mwanamke pekee aliyekuwa katika ajali hiyo pamoja na dereva wa baiskeli aliyejulikana kwa jina moja la Elvisa. Alisema mpaka sasa jeshi la polisi linamshikilia dereva wa gari ndogo (hiece) mpaka pale upelelezi utakapo kamilika.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Salashi Toure alisema kuwa wamepokea majeruhi 16 ambapo kati ya hao mmoja amehamishiwa katika hospitali ya Seliani baada ya mapafu yake kuvujia damu nyingi.