Basata kubana maadili kwa wasanii

Basta

Basata imekuja mkakati mwingine wa kuhakikisha kuwa wanaikomboa tasnia ya sanaa dhidi ya kupambana na maadili machafu katika filamu hususan tabia ya kuvaa na kukaa nusu uchi na kufanya mambo ya aibu yasiyovumilika. Basata inajipanga kuweka kanuni za adhabu ambazo zitadhibiti maadili katika filamu na wasanii wake kupitia mashirikisho husika.

Marais wa mashirikisho hayo ambao ni Symon Mwakifwamba (Filamu), Adrian Nyangamale (Ufundi), Ibra Washokera (Muziki) na Agnes Lukanga (Maonyesho), wamepanga kuhakikisha mipango madhubuti katika kuwafanya wasanii kuzingatia adhabu za vifungo vya muda mfupi na mrefu kwa wana sanaa ili wasishiriki katika kucheza filamu ambazo hazina maadili.

Marais hao waliweka wazi mikakati hiyo wakati wakiwasilisha mada kwa pamoja (Panel Discussion) kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii katika Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Baadhi ya mikakati iliyotajwa na marais hao ni ya kuhakikisha sheria ya hakimiliki na haki shiriki zinaangaliwa upya, kupambana na maharamia wa kazi za wasanii, kujenga mtandao mpana wa mashirikiano baina ya wasanii,kuimarisha uongozi wa vyama mbalimbali vya wasanii, kupambana na unyonyaji dhidi ya wasanii na kujenga maktaba za sanaa (Art Galleries) ambamo kazi mbali za sanaa zitahifadhiwa.

Rais Symon Mwakifwamba aliweka wazi kwamba, ’Kazi kubwa tulionayo ni kupambana na maharamia wa kazi zetu, kuandaa tuzo za filamu (people’s choice awards) ambazo zinatazamiwa kufanyika Februari mwakani, uvunjifu wa maadili na tabia chafu za wasanii wa filamu ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikilalamikiwa na wadau kiasi cha kuacha maswali mengi juu ya hatma ya wasanii wa tasnia hiyo.