Na Mwandishi Wetu,
RAIS Jakaya Kikwete amewasili salama nchini Tanzania leo akitokea nchini Marekani alipokuwa kwa matibabu ambapo alifanyiwa upasuaji kutibiwa saratani ya tezi dume katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyopo Baltimore, Maryland.
Akizungumza na wanahabari mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julias Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam alisema alipokuwa akiliarifu Baraza lake la Mawaziri kuwa anakwenda kutibiwa Saratani lilimshauri asitaje ugonjwa huo kwani utajenga hofu kubwa kwa Watanzania na kuwa na wasiwasi kwa rais wao.
Alisema yeye alikuwa tayari kutaja anachokwenda kutibiwa kabla ya kuanza safari lakini Baraza lake lilimsihi asifanye hivyo kwa kuhofia kujenga hofu kwa Wananchi. Alisema baada ya mvutano mrefu kikaoni alikubaliana na ushauri wa baraza lake na kwamba asitaje anachokwenda kufanyiwa ila umma ujulishwe kuwa Rais anakwenda kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.
Alisema ugonjwa aliyoenda kutibiwa (Saratani ya tezi dume) amekuwa akitembea nao zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuamua kwenda kufanyiwa matibabu hayo. Alishauri Watanzania wote kuwa na utaratibu wa kucheki afya zao mara kwa mara ili kuyatambua magonjwa yanayoweza kuwa yamejificha ndani ya mwili kabla ya kujitokeza. Hata hivyo baada ya kufanyiwa upasuaji na kumalizika salama aliomba Watanzania wajulishwe ili kuondoa wasiwasi.
“…Kukagua afya zetu ni suala muhimu sana, hata kwa magonjwa kama ya saratani…uzuri uchunguzi kama huu hata hapa Muhimbili (Hospitali ya Taifa ya Muhimbili) wanafanya upasuaji na kuchunguza magonjwa…” alisema Rais Kikwete.
Aidha Rais Kikwete ametoa shukrani kwa Watanzania wote waliokuwa wakimuombea na wengine kumtumia salamu za pole alipokuwa katika matibabu na kuwataka mungu awalipe na kuwazidishia upendo huo mara dufu, amewashukuru marais, viongozi mbalimbali wa dini na taasisi nyingine, familia yake na watu anuai ambao walikuwa pamoja kumjulia hali katika kipindi chote cha matibabu.
Hata hivyo amewashukuru madaktari wote walioshiriki katika matibabu yake kwa upendo na utaalamu wao waliouonesha kipindi chote na pia kutoa shukrani kwa wanahabari ambao walikuwa pamoja kuwajulisha Watanzania juu ya maendeleo ya afya yake nchini Marekani hali iliyojenga imani na matumaini kwao juu ya afya ya kiongozi wao.
“…Hakuna kitu kizuri na cha faraja kama unapokuwa katika matibabu hospitalini na kupata salam za pole, nashukuru sana kwa salam na maombi niliyotumiea…maana tulilazimika kutafuta simu na namba maalumu kupokea salamu baada ya simu yangu kuzidiwa…nilikuwa na pokea ujumbe wa pole (sms) takribani elfu 5000 kwa siku za salaam,” alisema Rais Kikwete.