Baraza la Biashara EAC Kuhamishia Makao Kigali

Mji wa Kigali nchini Rwanda pichani

Mji wa Kigali nchini Rwanda pichani

Na Mtuwa Salira, EANA

BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) litahamishia makao makuu yake mjini Kigali nchini Rwanda kutoka Arusha, Tanzania. Makao makuu ya sasa ya EABC ipo katika jengo binafsi la ghorofa moja eneo la Kijenge katika jiji la Arusha.

Kamati ya Utendaji ya EABC iliyoketi katika kikao chake maalum mjini Kigali Mei 30, mwaka huu kilipitisha azimio hilo  kwa mujibu wa mjumbe wa EABC, Lilian Awinja .

“Mkutano umeazimia mara moja kuendelea na mpango na utekelezaji wa ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya EABC Kigali,” alisema Awinja katika barua pepe aliyotuma kwa wanachama wa EABC na nakala yake kulipatia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).

Mkutano pia ulikubali ofa ya ardhi iliyotolewa na Tanzania mjini Arusha kutumika kama ofisi ya mawasiliano ya EABC. Ofa zote mbili za Rwanda na Tanzania zinafuatia maombi yaliyotolewa na EABC kwa nchi wanachama kwa ajili ya kupata maeneo ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya baraza hilo.

Kila nchi mwanachama itawasilishwa na mjumbu mmoja wa bodi isipokuwa Rwanda ambayo itawakilishwa na wajumbe wawili. Makao Makuu mapya ya EABC yanategemewa kuwa tayari katika kipindi cha miaka miwili.