Uongozi wa klabu ya Yanga umefanya mabadiliko ya nafasi za uongozi kwenye klabu hiyo mara baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga kubwaga manyanga.
Mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji ametoa taarifa rasmi ya maandishi inayoonesha mabadiliko hayo huku baadhi ya viongozi wakipanda wadhifa wakati wengine wakioneshwa mlango wa kutokea kwenye klabu hiyo.
Frank Chacha ndiye mwajiriwa pekee wa Yanga ambaye amepigwa chini baada ya ‘panga pangua’ hiyo wakati baadhi ya wafanyakazi wakibadilishwa vitengo huku wengine wakisalia kwenye nafasi zao za zamani.
Klabu inatangaza, mara moja kuwa: Baraka Deusdedit atashikilia nafasi hiyo ya Katibu Mkuu wa klabu.
Omar Kaya atachukua majukumu yanayohusiana na wanachama wa klabu. Pia atahakikisha anasimamia mikutano yote ya matawi, kusaidia maandalizi ya uchaguzi ujao pamoja na masuala ya wanachama wapya.
Jerry Muro ataendelea kubaki katika nafasi ya msemaji wa klabu, Faidhal Mike ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha cha Klabu, akisaidiwa na Justina ambaye amepandishwa cheo na kuwa mhasibu mkuu msaidizi.
Klabu ipo katika kipindi cha kuboresha kitengo cha masoko cha klabu na hivi karibuni itatangazwa lakini kabla ya hivyo, Omar atashikilia kwa muda kitengo hicho.
Mwanasheria Frank Chacha kama mkuu wa kitengo cha Sheria Klabuni, yeye tunamuacha aendelee na mambo yake na masuala yote ya kisheria, klabu itayafanya kutumia wanasheria, nje ya klabu.