Barabara ya Arusha-Namanga Yazinduliwa

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika uzinduzi rasmi wa Barabara ya Arusha – Namanga – Athi River yenye urefu wa kilometa 104.4 kwa upande wa Tanzania

Viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki Jumatano Novemba 28, 2012 wamefungua rasmi wa barabara ya Arusha – Namanga kwa upande wa Tanzania, na Namanga– Athi River kwa upande wa Kenya, kama sehemu ya mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi unaofanyika Nairobi, Kenya.

Barabara ya Arusha – Namanga – Athi River yenye urefu wa kilometa 104.4 kwa upande wa Tanzania ilikuwa ni mojawapo ya shughuli za uzinduzi rasmi wa Makao Makuu Mapya za Jumuiya uliofanyika mapema siku hiyo hiyo jijini Arusha, kabla ya viongozi hao kuelekea Athi River kwa ufunguzi wa barabara hiyo.

Ujenzi wa barabara ya Tanga–Horohoro, yenye urefu wa kilomita 66 pia nao umekamilika na tayari imeanza kurahishisha usafiri na usafirishaji baina ya Tanzania na Kenya na nchi nyingine wanachama.

Barabara nyingine zilizopo katika mtandao wa barabara wa Jumuiya zinazoendelea kujengwa kwa upande wa Tanzania, ni pamoja na zile za mtandao wa Dar es Salaam-Isaka-Lusahunga na Mutukula hadi Masaka; Lusahunga-Nyakasanza hadi Rusumo, na Rusumo-Kigali hadi Gisenyi.

Nyingine ni Biharamulo – Mwanza – Musoma – Sirari – Lodwar – Lokichogio; Tunduma – Sumbawanga – Kigoma – Manyovu (Mugina) – Rumonge – Bujumbura – Ruhwa (Bugarama) – Karongi hadi Gisenyi, pamoja na ile ya Tunduma – Iringa – Dodoma – Arusha – Namanga hadi Moyale.

Ujenzi wa barabara hizi utarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma baina ya nchi wanachama, na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji na vilevile gharama za kufanya biashara katika nchi za Jumuiya na hivyo kuvutia uwekezaji.